99
Mungu mtawala mkuu 1 Mwenyezi-Mungu anatawala, mataifa yanatetemeka! Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa, nayo dunia inatikisika! 2 Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni; ametukuka juu ya mataifa yote. 3 Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha. Mtakatifu ndiye yeye! 4 Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu! Umethibitisha haki katika Israeli; umeleta uadilifu na haki. 5 Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; angukeni kifudifudi mbele zake. Mtakatifu ndiye yeye! 6 Mose na Aroni walikuwa makuhani wake; Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia. Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza. 7 Alisema nao katika mnara wa wingu; waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa. 8 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza; kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao. 9 Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu; abuduni katika mlima wake mtakatifu! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.