24
Mfalme Mkuu(Zaburi ya Daudi) 1 Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu; ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake. 2 Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari; aliisimika imara juu ya mito ya maji. 3 Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu? Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu? 4 Ni mtu wa matendo mema na moyo safi, asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi, wala kuapa kwa uongo. 5 Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu, na haki yake kwa Mungu mwokozi wake. 6 Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye; naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo. 7 Fungukeni enyi milango; fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. 8 Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo; Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani. 9 Fungukeni enyi malango, fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. 10 Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi, yeye ndiye Mfalme mtukufu.