56
Kumtumainia Mungu(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Njiwa Mkimya wa Mbali”. Utenzi wa Daudi baada ya kukamatwa na Wafilisti kule Gathi) 1 Ee Mungu, unionee huruma, maana watu wananishambulia. Mchana kutwa maadui wananidhulumu. 2 Mchana kutwa maadui zangu wananishambulia; ni wengi mno hao wanaonipiga vita. 3 Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika, mimi nakutumainia wewe. 4 Namtumainia Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu dhaifu atanifanya nini? 5 Mchana kutwa wanapotosha kisa changu; mawazo yao yote ni ya kunidhuru. 6 Wanakutana kupanga na kunivizia; wanachunguza yote nifanyayo; wananiotea kwa shabaha ya kuniua. 7 Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao, uwaangushe hao waovu kwa hasira yako. 8 Wewe wakujua kusukwasukwa kwangu; waweka kumbukumbu ya machozi yangu yote. Je, yote si yamo kitabuni mwako? 9 Kila mara ninapokuomba msaada wako, maadui zangu wanarudishwa nyuma. Najua kweli Mungu yuko upande wangu. 10 Namtumaini Mungu na kusifu neno lake; namtumainia Mwenyezi-Mungu na kusifu neno lake. 11 Namtumainia Mungu, wala siogopi. Binadamu atanifanya nini? 12 Ee Mungu, nitatimiza ahadi zangu kwako; nitakutolea tambiko za shukrani, 13 Maana umeniokoa katika kifo, naam, umenilinda nisianguke chini; nipate kuishi mbele yako, ee Mungu, katika mwanga wa uhai.