64
Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi) 1 Usikie, ee Mungu, lalamiko langu; yalinde maisha yangu na vitisho vya maadui. 2 Unikinge na njama za waovu, na ghasia za watu wabaya. 3 Wananoa ndimi zao kama upanga, wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale. 4 Toka mafichoni wamshambulia mtu mnyofu, wanamshambulia ghafla bila kuogopa. 5 Wanashirikiana katika nia yao mbaya; wanapatana mahali pa kuficha mitego yao. Wanafikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona.” 6 Hufanya njama zao na kusema: “Sasa tumekamilisha mpango! Nani atagundua hila zetu?” Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu! 7 Lakini Mungu atawapiga mishale, na kuwajeruhi ghafla. 8 Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao; kila atakayewaona atatikisa kichwa. 9 Hapo watu wote wataogopa; watatangaza aliyotenda Mungu, na kufikiri juu ya matendo yake. 10 Waadilifu watafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, na kukimbilia usalama kwake; watu wote wanyofu wataona fahari.