52
Hukumu ya Mungu(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Daudi baada ya Doegi, Mwedomu, kumwendea Shauli na kumjulisha kuwa Daudi amekwenda nyumbani kwa Abimeleki) 1 Mbona, ewe jitu, wajivunia ubaya wako dhidi ya wenye kumcha Mungu? 2 Kila wakati unawaza maangamizi; ulimi wako ni kama wembe mkali! Unafikiria tu kutenda mabaya. 3 Wewe wapenda uovu kuliko wema, wapenda uongo kuliko ukweli. 4 Ewe mdanganyifu mkuu, wapenda mambo ya kuangamiza wengine. 5 Kwa hivyo Mungu atakuangamiza milele, atakunyakua na kukuondoa nyumbani mwako; atakungoa katika nchi ya walio hai. 6 Waadilifu wataona hayo na kuogopa, kisha watakucheka na kusema: 7 “Tazameni yaliyompata mtu huyu! Yeye hakutaka Mungu awe kimbilio lake; bali alitegemea wingi wa mali yake, na kutafuta humo usalama wake!” 8 Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu. Nazitegemea fadhili zake milele na milele. 9 Ee Mungu, nitakushukuru daima, kwa ajili ya mambo uliyofanya. Nitatangaza kwamba wewe ni mwema, mbele ya watu wako waaminifu.