Des 22 MAJILIO
MASOMO

SOMO 1: 1Sam.1:24-28
Siku zile, Hana alimchukua pamoja naye, na ng'ombe wa miaka mitatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.

WIMBO WA KATIKATI: 1Sam.2:1,4-8
1. Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; (K)

(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.

2. Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. (K)

3. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu. (K)

4. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;
Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana,
Naye ameuweka ulimwengu juu yake. (K)

Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Mfalme wa mataifa na jiwe la msingi wa Kanisa
uje kumwokoa mwanadamu aliyemuumba kwa udongo.
Aleluya.

INJILI: Lk.1:46-56
Siku ile Mariamu alisema,
Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;
Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.
Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi, Kwa hao wanaomcha.
Amefanya nguvu kwa mkono wake;
Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;
Na wanyonge amewakweza.
Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake;
Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele.
Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

------------

NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua sehemu ya sala za waamini

MAOMBI
Ndugu, Mkombozi wetu atakayekuja ni matunda ya huruma ya Mungu kufuatia kilio chetu tangu enzi za babu zetu. Kwa kuwa sasa anazidi kukaribia, tuombe:

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Kila mmoja wetu ajiandae kikamilifu na apewe ujasiri wa kukutana naye na kujitoa kwake kabisa.

2. Kwa kuwa kila tulicho nacho kimetoka kwako, utupe moyo wa kutoa chochote tulicho nacho kwa ajili yako na Kanisa lako Takatifu.

3. Ee Mungu Baba, rehema zako zadumu kizazi hata kizazi kwa wachaji wako. Uwakweze wanyonge, uwashibishe wenye njaa na utupe moyo wa kuhurumiana na kusadiana sisi kwa sisi.

4. Tunawaombea marehemu wetu F. ili wapokelewe huko aliko Mkombozi wetu.

Ee Baba mwema, Mwanao alivisikiliza vilio vya wengi: akina mama tasa, wajane na wengineo; kisha akawaonea huruma kwa kuwasaidia kadiri ya maombi yao. Kwa huruma yako, upokee maombi yetu tunayokutolea. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.