Des 18 MAJILIO
MASOMO

SOMO 1: Yer.23:5-8
Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu. Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri; lakini, Aishivyo Bwana, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.72:1-2,12-13,18-19
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani milele.

2. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na masikini,
Na nafasi za wahitaji ataziokoa. (K)

3. Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli,
Atendaye miujiza yeye peke yake;
Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;
Dunia yote na ijae utukufu wake.
Amina na amina. (K)

Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee kiongozi wa nyumba wa Israeli,
uliyempa Musa amri zako juu ya mlima Sinai,
uje kutuokoa kwa mkono wako.
Aleluya.

INJILI: Mt.1:18:24
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

------------

NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua sehemu ya sala za waamini

MAOMBI
Mkombozi wetu Yesu Kristo alizaliwa na Bikira Maria ili aukomboe uzao wa Ibrahimu. Leo Maria na Yosefu wanatukumbusha kuwa maisha ya wafuasi wa Kristo yanahitaji imani, matumaini na mapendo. Kwa hiyo, tuombe:

Kiitikio: Kwa huruma yako utusikie.
1. Kwa maombezi ya Bikira Maria na Mt.Yosefu, uwajalie watu wa ndoa uaminifu na mapendo ya kweli.

2. Utuweke chini ya maongozi yako hasa tunapopatwa na mashaka na hali ya kudhaniana vibaya.

3. Utujalie sisi sote kuheshimu ndoa za wenzetu, na watu wote wenye wito huo wafuate taratibu za Kanisa, ili kufikia kilele cha ndoa halali.

4. Uwaepushe na hatari zote watoto wote walio bado matumboni mwa mama zao, ili wazaliwe salama na kuondolewa dhambi ya asili kwa Ubatizo mtakatifu.

Ee Bwana, ili maombezi ya Yosefu na Maria yazae matunda, tunakiri kwamba sisi wenyewe yatupasa tuwe tayari kuvumiliana, kusameheana, kuombeana na kuepa kiburi, fitina au masengenyo yanayotutenga na upendo wako. Tujaliwe hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.