Des 17 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Mwa.49:2,8-10
Yakobo akawaita wanawe akawaambia; Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.
Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda
ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke;
ni nani atakaye mwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.72:1-4,7-8,17
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
2. Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, (K)
3. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)
4. Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Hekima ya Aliye juu,
unayepanga yote kwa nguvu zako na utaratibu mwema,
uje kutufunza njia ya busara.
Aleluya.
INJILI: Mt.1:1-17
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka
akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi
akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni
akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese;
Yese akamzaa mfalme Daudi. Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa
akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa
Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia
akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli. Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia
akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu;
Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa
Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa
YESU aitwaye Kristo. Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi
hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi
kumi na vinne.
------------
NOVENA YA NOELI
Kama inasaliwa hufuata mara baada ya Injili, na huchukua
sehemu ya sala za waamini
MAOMBI
Ndugu, Mkombozi atakayekuja ni Hekima ya Aliye juu, anayepanga yote kwa nguvu zake na utaratibu mwema.
Tumwombe Mungu, ili ujio wake utufunze njia ya busara:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kadiri Mkombozi anavyokaribia, viongozi wetu wa Kanisa waongezewe hekima yako na bidii, hasa katika
kuliandaa kiroho Taifa lako.
2. Atakapo kuja Yeye Mwenye milki, mataifa yote wamtambue na kumtii.
3. Upokee shukrani zetu kwa kutufanya uzao mteule unaotuunganisha kidugu na Yesu tangu Ibrahimu, na
uwape neema zako wale watakaozaliwa upya kwa Ubatizo siku ya Noeli.
4. Ndugu zetu marehemu F. wapokelewe kifuani pa Ibrahimu na kulakiwa na malaika
wako watakatifu.
Ee Mungu, wewe ni Bwana wa vizazi vyote, utujalie hekima na imani kama ya mzee wetu Ibrahimu, ili tustahili
kuitwa wakombolewa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.