ALHAMISI KUU MISA YA JIONI
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Gal.6:14
Lakini sisi yatupasa kuona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndani yake
mna wokovu, uzima na ufufuko wetu, nasi tumeokolewa na kusalimishwa naye.
UTUKUFU husema:
Wakati huo kengele hupigwa, Wimbo ukiisha kengele hunyamaa mapaka
Kesha la Pasaka, isipokuwa Askofu wa Jimbo ameagiza vinginevyo kwa sababu ya kufaa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, tumekusanyika ili kuadhimisha Karamu takatifu sana ambamo Mwanao, kabla ya kutolewa afe,
alilikabidhi Kanisa kwa karne zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake. Tunakuomba utujalie, tupate
kuchota katika fumbo hili kuu utimilifu wa mapendo na uzima. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu milele na milele.
SOMO 1: Kut.12:1-8,11-14
Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi za Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi
kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku
ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwanakondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwanakondoo kwa
watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwanakondoo, basi yeye na jirani yake
aliye karibu na nyumba yake na watwae mwanakondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu, kwa kadiri ya
ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwanakondoo. Mwanakondoo wenu atakuwa
hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya
kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa
baadhi ya damu yake na kutia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba
watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu;
tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi: mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu
vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita
kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa
mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile
damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu
yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho
kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri
ya milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:12-13,15-18
1. Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Kikombe kile cha Baraka tukibarikicho,
Je! Si ushirika wa damu ya Kristo?
2. Ina thamani machoni pa Bwana,
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako.
Umevifungua vifungo vyangu. (K)
3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)
SOMO 2: 1Kor.11:23-26
Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa
alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili
yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akikitwaa kikombe, akisema,
Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.
Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
SHANGILIO: Yn.13:34
Amri mpya nawapa,
Mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi,
asema Bwana.
INJILI: Yn.13:1-15
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika
ulimwengu kwenda kwa Baba, naye aliwapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati
wa chakula cha jioni, naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti;
Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na yakuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda
kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha
akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.
Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia,
Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe.
Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu,
hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya
kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye
atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa
mavazi yake, na kuteti tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita Mwalimu,
na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha
miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi
nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Yesu Kristo alituachia wosia wake katika tukio la kuweka Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu, siku moja kabla ya mateso yake. Leo tunapoadhimisha fumbo hilo, tunayo haya ya kumwomba
Mungu. Ee Baba wa huruma tunakuomba:
1. Uwajalie wote wenye Daraja Takatifu katika Kanisa lako kudumu kiaminifu katika wito huu mtakatifu;
na wawahudumie ndugu zao kwa upendo usio na mipaka.
2. Utusaidie kuadhimisha Ekaristi Takatifu kwa uchaji na kwa ibada kubwa; na utujalie neema ya
kuunganika na Mwanao ambaye hutulisha, hutunywesha, hututuliza na kutuongoza.
3. Utupe mwanga wako wa Pasaka ili tuyatambue mapendo yako; na tuweze kuyaunganisha matatizo yetu
na Sadaka ya Mwanao.
4. Utujalie bidii ya kushiriki adhimisho la Misa Takatifu mara nyingi, tupate nguvu ya kudumu
katika imani, matumaini na mapendo ya kweli.
5. Uwaite vijana wengi katika miito yako mitakatifu, na uwajalie neema tele wale wote walioitikia
miito hiyo kwa ajili ya kulihudumia Kanisa lako.
6. Sisi sote tuwe tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya kuwasaidia wenzetu, wazima na wafu, katika
taabu zao.
Ee Mungu wa mapendo, kwa Ubatizo umetushirikisha ukuhani wa Mwanao tupate kulieneza pendo lako
kwa wanadamu wote. Uipokee sala yetu na kutuneemesha zaidi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie kushiriki kwa heshima mafumbo haya, kwani, kila tunapoadhimisha
ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka. Tunaomba haya kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI
Sadaka na sakramenti ya Kristo
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote,
ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye aliye Kuhani wa kweli na wa milele, alipoweka utaratibu wa sadaka hii ya kudumu alijitoa wa
kwanza kwako kafara ya kuleta wokovu akatuagiza na sisi tuitoe kwa kumkumbuka Yeye.
Nasi tunaimarishwa, tupokeapo mwili wake uliotolewa sadaka kwa ajili yetu, na tunatakaswa tuinywapo
damu yake iliyomwagika kwa ajili yetu.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu
wako, tukisema bila mwisho.
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu...
ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.11:24-25
Huu ndio Mwili wangu ulio kwa ajili yenu. Kikombe hiki ni agano jipya katika Damu yangu, asema
Bwana. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, kama vile tunavyotiwa nguvu na Karamu ya Mwanao hapa duniani, vivyo hivyo
utujalie tustahili kushiba katika karamu ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.