ALHAMISI KUU MISA YA KRISMA
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Ufu.1:6
Yesu Kristo ametufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu
na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.
Utukufu husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, umempaka mafuta Mwanao pekee kwa Roho Mtakatifu, na ukamfanya Kristo na Bwana. Uwe
radhi kutujalia ili, tukiisha kushirikishwa utakatifu wake, tuwe mashahidi wa Ukombozi ulimwenguni.
Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.61:1-3,6.8-9
Roho ya Bwana Mungu i juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari
njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa
habari za kufunguliwa kwao; kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu;
kuwafariji wote waliao, kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito. Nanyi mtaitwa makuhani wa
Bwana, watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu.
Mimi nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele. Na kizazi chao kitajulikana katika
mataifa, na uzao wao katika kabila za watu. Wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa
na Bwana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.89:20-21,24.26;(K)
1. Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
Nimempaka mafuta yangu matakatifu;
Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
Na mkono wangu utamtia nguvu.
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
2. Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo,
Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
Yeye ataniita, Wewe Baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu. (K)
SOMO 2: Ufu.1:5-8
Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza
wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa
Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na
mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili
yake. Naam. Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako
na atakayekuja, Mwenyezi.
SHANGILIO: Lk.4:18
Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwa maana amenitia mafuta,
amenituma kuwahubiri maskini habari njema.
INJILI: Lk.4:16-21
Wakati ule, Yesu alikwenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika inagogi
kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.
Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua, akatafuta mahali palipoandikwa: “Roho wa Bwana
yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza
mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo
katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, "Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu".
KUWEKA TENA AHADI ZA KIPADRI
Baada ya homilia, Askofu anawaambia mapadri maneno kama haya:
Askofu:
Wanangu wapendwa sana, tunakumbuka pia mwaka huu ile siku Bwana wetu Yesu Kristo alipowapa
Mitume upadri wake na kutupa sisi pia. Je, mwataka kuweka tena ahadi mlizotoa zamani mbele
ya Askofu wenu na mbele ya waamini?
Mapadri:
Ninataka!
Askofu:
Je, mwataka kuunganika zaidi na Bwana Yesu na kufanana naye, kwa kujikana wenyewe
na kuzithibitisha ahadi za majukumu yenu matakatifu, ambayo, mkisukumwa na upendo wa
Kristo, mliyapokea kwa furaha kwa ajili ya Kanisa lake siku mlipopewa upadri?
Mapadri:
Ninataka!
Askofu:
Je, mwataka kuwa wagawaji waaminifu wa mafumbo ya Mungu kwa njia ya Ekaristi takatifu na
maadhimisho mengine ya kiliturujia, na kutekeleza kwa uaminifu jukumu la kufundisha, mkimfuata
Kristo, aliye Kiongozi na Mchungaji, siyo kwa tamaa ya mali, bali mkisukumwa tu na juhudi ya
kutaka kuwaokoa watu?
Mapadri:
Ninataka!
Kisha Askofu anawaelekea watu na kuwaambia:
Askofu:
Nanyi pia, wanangu waamini wapendwa sana, waombeeni mapadri wenu, ili Bwana awashushie wingi
wa mema yake, wapate kuwa watumishi waaminifu wa Kristo, Kuhani mkuu, wawafikisheni kwake Yeye
aliye asili ya wokovu.
Waamini:
Kristo, utusikie. Kristo, utusikilize.
Askofu:
Niombeeni na mimi pia, nipate kuwa mwaminifu katika jukumu la kitume nililokabidhiwa katika
unyonge wangu, niwe kati yenu, siku kwa siku, mfano ulio hai na mkamilifu zaidi wa Kristo
aliye Kuhani, Mchungaji Mwema, Mwalimu na Mtumishi wa wote.
Waamini:
Kristo, utusikie. Kristo, utusikilize.
Askofu:
Bwana na atulinde sote katika upendo wake, naye mwenyewe atufikishe sote, wachungaji pamoja
na kondoo, kwenye uzima wa milele.
Waamini:
Amina.
Nasadiki haisemwi.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba ili nguvu za sadaka hii zituepushe na utumwa wetu wa zamani na
kutuzidishia uzima mpya na wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI:
Ukuhani wa Kristo na huduma ya kikuhani.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na
popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Ulimweka Mwanao pekee aliyepakwa mafuta na Roho Mtakatifu kuwa Kuhani mkuu wa agano jipya na
la milele. Ukapenda, kwa mpango wa ajabu, ukuhani wake pekee udumu katika Kanisa. Maana yeye
mwenyewe analipamba taifa alilojipatia kwa ukuhani wa kifalme; na kwa wema wa kindugu amewateua
pia watu ili washirikishwe huduma yake takatifu kwa kuwekewa mikono. Nao, katika jina lake,
waendelee kuadhimisha sadaka ya ukombozi wa wanadamu, wakiandaa karamu ya kipasaka kwa ajili
ya wana wako; walitangulie taifa lako takatifu katika mapendo, walilishe kwa neno lako na kuwatia
uzima kwa sakramenti. Nao, wakitoa nafsi zao kwa ajili yako na kwa wokovu wa ndugu zao, wajitahidi
kufanana na sura ya Kristo mwenyewe; na wadumu katika kushuhudia imani na upendo kwako.
Kwa hiyo, ee Bwana, sisi nasi pamoja na Malaika na Watakatifu wote, tunakusifu, tukisema kwa
shangwe:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu...
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.89:1
Fadhili za Bwana nitaziimba milele, kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba kwa unyenyekevu, uwafanye hao unaowalisha kwa sakramenti zako
waeneze ulimwenguni harufu nzuri ya Kristo. Anayeishi na kutawala milele na milele.