BWANA WETU YESU KRISTO MFALME WA ULIMWENGU
MASOMO MWAKA C
ANTIFONA YA KUINGIA: Ufu.5:12;1:6
Astahili Mwanakondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima. Utukufu na ukuu una
Yeye hata milele na milele.
Utukufu husemwa
KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi wa milele, umependa kuvifanya upya vitu vyote katika Mwanao mpenzi, Mfalme wa ulimwengu. Uwe
radhi kuvijalia viumbe vyote, vilivyokombolewa katoka utumwani, vipate kukutumikia katika fahari yako na kukusifu
bila mwisho. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
Mungu, milele namilele.
SOMO 1: 2Sam.5:1-3
Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na
nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na
kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi, wazee
wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia
Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.122:1-5, (K)1
1. Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani mwa Bwana.
Miguu yetu imesimama,
Ndani ya malango yako ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
2. Ee Yerusalemu uliyejengwa,
Kama mji ulioshikamana;
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)
3. Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko huko viliwekwa viti vya hukumu,
vya enzi vya nyumba ya Daudi. (K)
SOMO 2: Kol.1:11-20
Mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu
pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye
alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye
tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi. Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa
kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana, ikiwa
ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako
kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo,
ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote
ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa
ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
SHANGILIO: Mk.11:10
Aleluya, aleluya!
Abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana:
Ubarikiwe na Ufalme ujao, wa baba yetu Daudi.
Aleluya!
SOMO 3: INJILI: Lk.23:35-43
Watu walisimama wakimtazama Yesu. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe
mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,
huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani: HUYU NDIYE MFALME
WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.
Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki
kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tulivyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. Kisha
akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, makuambia, leo hivi utakuwa pamoja
nami peponi.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Neno zuri kupita maneno yote lilikuwa neno lile la Yesu alilomwambia jambazi mmoja aliyesulibiwa pamoja naye: leo hivi
utakuwa pamoja nami paradisini. Ee Bwana Yesu Kristo,
1. Tunakuomba sana utusaidie kutambua uwepo wako katika maisha yetu ya kila siku.
2. Utupe moyo wa toba ili kujitayarisha kuwa nawe paradisini.
3. Utuongoze katika njia za maisha yetu hapa duniani tusipotee.
4. Utusaidie kutumia vitu na mali za dunia hii kama msaada wa kutufikisha kwako.
5. Utukumbushe kwamba maisha ya duniani yatakwisha na kwamba tumeumbwa kuishi milele katika heri ya uzima wa milele.
Ee Mungu Baba, Mwana wako kweli ni mfalme anayeangalia sana mahitaji yetu. Anatutayarishia mahali pa kukaa katika
ufalme wa Milele. Uyapokee maombi yetu kwa njia yake yeye anayeishi na kutawala katika ufalme wako daima na milele.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, huku tukikutolea kafara ya upatanisho wa wanadamu wote, tunakusihi kwa unyenyekevu ili
Mwanao mwenyewe awajalie mataifa yote zawadi za umoja na amani. Anayeishi na kutawala milele na milele.
UTANGULIZI
Kristo mfalme wa ulimwengu
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote,
ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe ulimpaka mafuta ya furaha Mwanao pekee, Yesu Kristo Bwana wetu, awe Kuhani wa milele na
Mfalme wa ulimwengu wote.
Alijitoa mwenyewe juu ya altare ya msalaba awe kafara safi iletayo amani, ili atimize mafumbo
ya ukombozi wa watu.
Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na
wa ulimwengu wote; ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki,
upendo na amani.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki,
na pamoja na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema
bila mwisho:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ...
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.29:10,11
Bwana ameketi hali ya mfalme milele; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Baada ya kupokea chakula cha uzima wa milele, tunakuomba, ee Bwana, ili sisi, tunaoona fahari
kuzitii amri za Kristo Mfalme wa ulimwengu, tuweze kuishi bila mwisho pamoja naye katika ufalme
wa mbinguni. Anayeishi na kutawala milele na milele.