UTATU MTAKATIFU MWAKA C MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA.
Ahimidiwe Mungu Baba, na Mwanawe pekee, na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametutendea rehema yake.
Utukufu husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu Baba, kwa kumpeleka ulimwenguni Neno wa ukweli na Roho wa utakatifuzo, uliwafumbulia
wanadamu fumbo lako la ajabu. Utujalie ili, katika kuungama imani ya kweli, tuutambue utukufu
wa Utatu Mtakatifu wa milele, na tuuabudu Umoja wake katika enzi ya fahari yake. Kwa njia ya
Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu,
Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mit.8:22-31
Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale, Nalitukuka tokea
milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako
chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa; Alipokuwa
hajaiumba dunia, wala makonde, Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako;
Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari
zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza
misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku;
Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja
na wanadamu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.8:3-8(K)1
1. Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha,
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
(K) Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
2. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
3. Kondoo, na ng'ombe wote pia,
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za baharini. (K)
SOMO 2: Rum.5:1-5
Tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana
wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama
ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na tufurahi
katika dhiki pia; tukijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti
wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo
la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
SHANGILIO: Ufu.1:8
Aleluya, aleluya!
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Mungu aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja.
Aleluya!
INJILI: Yn.16:12-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili
hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote,
kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo
atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha
habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo tu
yangu, na kuwapasheni habari.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Waumini wenzangu, Mungu ni mkubwa apitaye ufahamu wetu. Tunamfahamu Mungu kadiri anavyojifunua kwetu
katika viumbe vyake, ukombozi wake na kazi ya Roho Mtakatifu. Tumuombe Mungu Baba,
1. Ee Mungu Mkuu: Ulisaidie Kanisa lako kulitunza na kuliheshimu fumbo la Utatu Mtakatifu kama hazina
kubwa ya imani yetu.
2. Uwongoze watu wote duniani kukuheshimu na kukuabudu kama mwumbaji wao.
3. Uwahimize watawala wa dunia kuheshimu na kutunza haki za kibinadamu.
4. Ufungue mioyo ya watu wote na Uwasaidie kukutambua Wewe uliye Mungu uwapendao.
5. Utusaidie sisi wakristo kukuungama Wewe bila hofu mbele ya watu wote.
6. Uwajalie marehemu wetu waliokutegemea katika maisha yao ya hapa duniani kuonja huruma na wema
wako.
Ee Mungu mmoja katika nafsi tatu, uyasikilize maombi yetu tunayokutolea kwa njia ya Bwana wetu
Yesu Kristo, anayeishi na kutawala pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu daima na milele. Amina.
UTANGULIZI: Fumbo la Utatu Mtakatifu
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee
Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe pamoja na·Mwanao pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa
nafsi, ila katika Utatu wa umungu mmoja.
Mambo tunayoyasadiki juu ya utukufu wako, kwa sababu ya ufunuo wako, twayasadiki pia juu ya
Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana. Nasi tunapoungama Umungu wa kweli
na wa milele, tunaabudu nafsi zilizo mbalimbali za Mungu mmoja zenye utukufu ulio sawa.
Nao Malaika na Malaika wakuu, Makerubi na Maserafi wote hawachoki kukusifu kila siku, wakisema
kwa sauti moja:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Gal.4:6
Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba,
yaani, Baba.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana Mungu wetu, sakramenti hii tuliyoipokea ituletee afya ya mwili na roho, na kutuwezesha
kuungama Umoja wa Mungu katika Utatu Mtakatifu wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.