
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu
Kabla ya Adhuhuri:
ANT.: Tunakuomba, tunakusifu, tunakuabudu, Ee Utatu Mtakatifu.
Adhuhuri:
ANT.: Ee Utatu Mtakatifu, wewe ni tumaini letu, wokovu wetu na utukufu wetu.
Baada ya Adhuhuri:
ANT.: Tunakiri kwamba kwako wewe, daima ni tendo moja: kuwa, kuishi na kujua.
Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi
(mate.4:11)
I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.
Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?
Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.
Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.
Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.
Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!
Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"
Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.
Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!
Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.
Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.
Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.
Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.
Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.
Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.
Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.
Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.
Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri:
ANT.: Tunakuomba, tunakusifu, tunakuabudu, Ee Utatu Mtakatifu.
Adhuhuri:
ANT.: Ee Utatu Mtakatifu, wewe ni tumaini letu, wokovu wetu na utukufu wetu.
Baada ya Adhuhuri:
ANT.: Tunakiri kwamba kwako wewe, daima ni tendo moja: kuwa, kuishi na kujua.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 2Kor.1:21-22
Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka
wakfu; ndiye aliyetutia muhuri wa kuwa mali yake yeye, na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama
dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
K. Ingieni kwake kwa kelele za shangwe.
W. Mtukuzeni Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Gal.4:4,5-6
Wakati ule maalum ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini
ya Sheria, apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.
Kwa vile sasa ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia
"Abba," yaani "Baba."
K. Tunakuomba, Ee Utatu Mtakatifu, mbarikiwa na mtukufu.
W. Baba, Mwana, Roho Mtakatifu, utusikie.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Ufu.7:12
Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na
milele! Amina.
K. Bwana, umetukuzwa juu ya mbingu.
W. Milele umehimidiwa na kusifiwa kuliko vingine vyote.
SALA:
Tuombe: Mungu Baba yetu, uliwafumbulia watu fumbo kuu la umungu wako pale ulipowatuma ulimwenguni
Neno ambaye ni Ukweli, na Roho ambaye hututakatifuza. Utusaidie tuweze kukusadiki na kukuabudu,
kama imani ya kweli inavyofundisha: Nafsi tatu, zenye utukufu milele, Mungu mmoja, mwenye enzi
isiyopimika. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.