
MASIFU YA JIONI II
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina, Aleluya.
UTENZI
Ninasadiki kweli na kwa dhati
Mungu ni Mmoja, Nafsi Tatu;
Na halafu ninakiri kabisa
Mwana ubinadamu alitwaa;
Nguvu na tumaini langu lote.
Ni kwa utu uliosulibiwa;
Kila wazo na tendo lisofaa
Ni mauti, kama alivyokufa.
Nuru na uzima na nguvu yote
Hutokana tu na neema yake;
Nampenda sana sana yeye tu,
Bwana mtakatifu, mwenye nguvu.
Pamoja na Jeshi la malaika,
Na kwa njia yao tutoe sifa
Kwa Mungu wa dunia na wa mbingu,
Baba, Mwana, Roho Mtakatifu.
ANT. I: Ewe Utatu halisi, uliye juu kabisa na wa milele, Baba, Mwana
na Roho Mtakatifu.
Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini
ya miguu yake (Kor.15:25)
Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,
Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."
Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"
Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.
Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.
Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.
Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Ewe Utatu halisi, uliye juu kabisa na wa milele, Baba, Mwana
na Roho Mtakatifu.
ANT. II: Ewe Utatu Mtakatifu, utupatie uhuru, wokovu na uzima.
Zab.114:1-8 Mungu pamoja na watu wake
Nanyi mliouacha ulimwengu huu, tambueni kuwa mmeokolewa kutoka Misri
(Mt. Augustino)
Watu wa Israeli walipoondoka nchini Misri,*
wazao wa Yakobo walipotoka ugenini,
Yuda likawa taifa takatifu la Mungu,*
Israeli ikawa mali yake mwenyewe.
Bahari ya Shamu iliona ikakimbia;*
mto Yordani ukaacha kutiririka!
Milima ilirukaruka kama kondoo dume,*
vilima vikaruka kama wana-kondoo!
Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?*
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?
Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?*
Nanyi vilima, imekuwaje mkaruka kama wanakondoo?
Tetemeka, ewe dunia, mbele yake Mungu;*
Naam, mbele ya Mungu wa Yakobo,
anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,*
nayo majabali yakawa chemchemi za maji.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Ewe Utatu Mtakatifu, utupatie uhuru, wokovu na uzima.
ANT. III: Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu Bwana Mungu Mwenyezi,
aliyekuwako, aliyeko, na atakayekuja.
WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo
Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi, ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).
ANT. III: Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu Bwana Mungu Mwenyezi,
aliyekuwako, aliyeko, na atakayekuja.
SOMO: Ef.4:3-6
Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna
mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja,
imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya
kazi katika yote na yuko katika yote.
KIITIKIZANO
K. Tumtukuze Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Tumsifu Mungu milele. (W. Warudie)
K. Atukuzwe na kuheshimiwa Mungu peke yake.
W. Tumsifu Mungu milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tumtukuze...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Kwa moyo na midomo yetu tunakusifu, tunakuabudu na kukutukuza wewe, Mungu: Baba usiye na baba,
Mwana wa pekee, na Roho Mtakatifu Mfariji; utukufu wote uwe kwako milele.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Kwa moyo na midomo yetu tunakusifu, tunakuabudu na kukutukuza
wewe, Mungu: Baba usiye na baba, Mwana wa pekee, na Roho Mtakatifu Mfariji; utukufu wote uwe
kwako milele.
MAOMBI
Baba, kwa njia ya Roho wako Mtakatifu, ulitujalia Mwanao Kristo azaliwe kwetu, ili tuweze kupata
uzima kwa njia yake. Tukiwa tumejaa sasa uzima huo, twainua mioyo yetu kuusifu Utatu Mtakatifu,
tukisema:
W. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
Baba Mwenyezi, Mungu wa milele, kwa jina la Mwanao uliletee Kanisa Roho wako Mtakatifu:
- tunaomba huyo Mfariji atudumishe katika umoja, uelewano na ukweli kamili. (W.)
Bwana, uwapeleke wafanyakazi wako shambani, ili wakawafundishe watu wa mataifa yote, na kuwabatiza
kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu:
- uwaimarishe wote katika imani. (W.)
Bwana, uwasaidie wale wote ambao wanadhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Mwanao:
- uwapatie Roho wa ukweli ambaye atasema kwa njia yao, kama Mwanao alivyoahidi. (W.)
Baba Mwenyezi, wote wanakiri kuwa wewe, Neno na Roho ni mmoja:
- kama tunavyoamini katika wewe, Mungu mmoja, vivyo hivyo tukutumainie na kukupenda. (W.)
Baba wa walio hai, uwashirikishe wote waliofariki dunia utukufu wako:
- uwawezeshe kutawala milele mbinguni pamoja nawe, na Mwanao, na Roho Mtakatifu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Baba yetu, uliwafumbulia watu fumbo kuu la umungu wako pale ulipowatuma ulimwenguni Neno
ambaye ni Ukweli, na Roho ambaye hututakatifuza. Utusaidie tuweze kukusadiki na kukuabudu, kama
imani ya kweli inavyofundisha: Nafsi tatu, zenye utukufu milele, Mungu mmoja, mwenye enzi
isiyopimika. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.