
MASIFU YA JIONI I
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Ninasadiki kweli na kwa dhati
Mungu ni Mmoja, Nafsi Tatu;
Na halafu ninakiri kabisa
Mwana ubinadamu alitwaa;
Nguvu na tumaini langu lote
Ni kwa utu uliosulibiwa;
Kila wazo na tendo lisofaa
Ni mauti, kama alivyokufa.
Nuru na uzima na nguvu yote
Hutokana tu na neema yake;
Nampenda sana sana yeye tu,
Bwana mtakatifu, mwenye nguvu.
Pamoja na jeshi la malaika,
Na kwa njia yao tutoe sifa
Kwa Mungu wa dunia na wa mbingu,
Baba, Mwana, Roho Mtakatifu.
ANT. I: Utukufu wote ni mali yako, Ewe Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja,
kabla sasa na hata milele ya nyakati zote,
Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!
Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.
Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!
Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.
lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.
Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;
Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,
na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.
Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Utukufu wote ni mali yako, Ewe Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja,
kabla sasa na hata milele ya nyakati zote,
ANT. II: Utukuzwe Utatu Mtakatifu na umoja usiogawanyika; tumsifu
Mungu, kwa kuwa ametuonesha huruma.
Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, ee Sion!
Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.
Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.
Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.
Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu
Huleta mvua ya mawe,/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.
Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.
Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.
Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Utukuzwe Utatu Mtakatifu na umoja usiogawanyika; tumsifu
Mungu, kwa kuwa ametuonesha huruma.
ANT. III: Utukufu na heshima viwe kwa Mungu, katika umoja wa Utatu;
kwa Baba na kwa Mwana, pamoja na Roho Mtakatifu, daima na milele.
WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Utukufu na heshima viwe kwa Mungu, katika umoja wa Utatu;
kwa Baba na kwa Mwana, pamoja na Roho Mtakatifu, daima na milele.
SOMO: Rom.11:33-36
Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki!
Kama yasemavyo Maandiko matakatifu: "Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa
mshauri wake? Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kukilipwa tena kitu hicho?" Kwa maana
vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata
milele! Amina.
KIITIKIZANO
K. Tumtukuze Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Tumsifu Mungu milele. (W. Warudie)
K. Atukuzwe na kuheshimiwa Mungu peke yake.
W. Tumsifu Mungu milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Tumtukuze...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Tunakushukuru, Ewe Mungu; tunakushukuru wewe uliye mmoja na Utatu halisi, uliye Mungu mmoja na
wa juu kabisa, uliye mmoja na Umoja mtakatifu kabisa.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Tunakushukuru, Ewe Mungu; tunakushukuru wewe uliye mmoja na
Utatu halisi, uliye Mungu mmoja na wa juu kabisa, uliye mmoja na Umoja mtakatifu kabisa.
MAOMBI
Baba, kwa njia ya Roho wako Mtakatifu, ulitujalia Mwanao Kristo azaliwe kwetu, ili tuweze kupata
uzima kwa njia yake. Tukiwa tumejaa sasa uzima huo, twainua mioyo yetu kuusifu Utatu Mtakatifu,
tukisema:
W. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
Baba Mwenyezi, Mungu wa milele, kwa jina la Mwanao uliletee Kanisa Roho wako Mtakatifu:
- tunaomba huyo Mfariji atudumishe katika umoja, uelewano na ukweli kamili. (W.)
Bwana, uwapeleke wafanyakazi wako shambani, ili wakawafundishe watu wa mataifa yote, na kuwabatiza
kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu:
- uwaimarishe wote katika imani. (W.)
Bwana, uwasaidie wale wote ambao wanadhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Mwanao:
- uwapatie Roho wa ukweli ambaye atasema kwa njia yao, kama Mwanao alivyoahidi. (W.)
Baba Mwenyezi, wote wanakiri kuwa wewe, Neno, na Roho ni mmoja:
- kama tunavyoamini katika wewe, Mungu mmoja, vivyo hivyo tukutumainie na kukupenda. (W.)
Baba wa walio hai, uwashirikishe wote waliofariki dunia utukufu wako:
- uwawezeshe kutawala milele mbinguni pamoja nawe, na Mwanao, na Roho Mtakatifu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Baba yetu, uliwafumbulia watu fumbo kuu la umungu wako pale ulipowatuma ulimwengu Neno
ambaye ni Ukweli, na Roho ambaye hututakatifuza. Utusaidie tuweze kukusadiki na kukuabudu,
kama imani ya kweli inavyofundisha: Nafsi tatu, zenye utukufu milele, Mungu mmoja, mwenye
enzi isiyopimika. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na
kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.