Generic placeholder image

JUMAPILI YA PENTEKOSTE
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Roho Mtakatifu alishuka kutoka kiti cha enzi cha Mungu, na bila ya kuonekana, akaingia mioyoni mwa mitume, aleluya.

Adhuhuri
Ant.: Bwana, tunaomba utuongezee imani, na uifanye nuru ya Roho Mtakatifu ituangaze daima, aleluya.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Si ninyi mtakaokuwa mnasema, bali Roho wa Baba yenu atakuwa anasema ndani yenu, aleluya.

Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi (mate.4:11)

I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."

Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.

Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?

Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.

Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.

Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.

Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.

Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.

Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!

Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"

Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.

Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!

Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.

Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.

Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.

Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.

Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.

Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!

Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.

Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.

Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Roho Mtakatifu alishuka kutoka kiti cha enzi cha Mungu, na bila ya kuonekana, akaingia mioyoni mwa mitume, aleluya.

Adhuhuri
Ant.: Bwana, tunaomba utuongezee imani, na uifanye nuru ya Roho Mtakatifu ituangaze daima, aleluya.

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Si ninyi mtakaokuwa mnasema, bali Roho wa Baba yenu atakuwa anasema ndani yenu, aleluya.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.12:13
Sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.

K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya.
W. Atawafudisheni mambo yote, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Tito3:5b-7
Mungu alitukomboa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mkombozi wetu, ili kwa neema yake tupate uhusiano mwema na Mungu, na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.

K. Roho Mtakatifu atawafundisheni, aleluya.
W. Ndipo mtaelewa yote ambayo nimewaambieni, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.1:21-22
Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi ha ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; ndiye aliyetutia muhuri wa kuwa mali yake yeye, na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.

K. Mitume walisema lugha mbalimbali, aleluya.
W. Waliyatangaza matendo makuu ya Mungu, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, utuangaze kwa mng'ao wa utukufu wako. Kristo, ambaye ni nuru kutoka nuru yako, na aimarishe, kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu, mioyo ya wale waliozaliwa upya kwa neema. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.