PENTEKOSTE
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Hek.1:7
Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviungamanisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, aleluya!

Au:
Rum.5:5;8:11

Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu kwa Roho wake anayekaa ndani yetu, aleluya!

Utukufu husemwa.

KOLEKTA

Ee Mungu, kwa njia ya fumbo la sherehe ya leo, unalitakatifuza Kanisa lako lote lililoenea katika kila kabila na taifa. Umimine vipaji vya Roho Mtakatifu katika ulimwengu wote, na, yale yaliyotendwa kwa neema yako mwanzoni mwa kuihubiri Injili, uyaeneze pia sasa mioyoni mwa waamini. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.2:1-11
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.104:1,24,29-31,34,(K)30
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)

(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana,
Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Au:
Aleluya.

2. Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

3. Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

SOMO 2: 1Kor.12:3b-7,12-13
Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Kristo, Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka;
Basi na tuifanye karamu katika Bwana!
Aleluya!

INJILI: Yn.20:19-23
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Yesu aliyefufuka hakufungwa tena kwa pingu za mahali na wakati. Kwa njia hiyo aliwaonesha mitume wake enzi na mamlaka yake yote mbinguni na duniani.

Tuombe,
1. Utujalie nguvu ya Roho Mtakatifu ili atuongoze katika njia za maisha yetu siku zote.

2. Roho Mtakatifu ni Roho wa amani. Utujaze nia ya kudumisha amani katika mazingira yetu.

3. Roho Mtakatifu ni Roho wa upendo: Uondoe mioyoni mwetu chuki, fitina, hila na udanganyifu.

4. Roho Mtakatifu ni Roho wa umoja: Utuunganishe sisi wenye imani moja katika umoja wa maisha ya kusaidiana na kushirikiana.

5. Roho huyo ni Roho wa upole: Utuongoze katika kutafuta njia za upole na za kupatana na wenzetu.

6. Roho huyo anasali ndani yetu: Utupe neema ya kusikiliza sauti yake inayotusukuma kutenda mema na kukufuata.

7. Roho huyo ni dhamiri yetu: Utuangaze tufuate uongozi wake tusipotee katika njia ya kufika kwako.

Ee Mungu Baba, katika uongozi wako ulipanga mambo mengi ya ajabu. Mwana wako ametukomboa katika nguvu za ubaya na dhambi. Roho wako anaendeleza kazi ya ukombozi wetu. Upokee maombi yetu tunayotamka kwa uongozi wa Roho Mtakatifu anayeishi na kutawala nawe na Mwana wako milele. Amina

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba utujalie ili, kama alivyoahidi Mwanao, Roho Mtakatifu atufunulie zaidi siri ya sadaka hii, na kwa huruma yake atufumbulie kweli yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Fumbo la Pentekoste.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Leo umetimiza fumbo la Pasaka na kuwajalia Roho Mtakatifu wale uliowafanya kuwa wanao kwa kuwaunganisha na Mwanao pekee.
Hapo mwanzo wa Kanisa, huyo Roho Mtakatifu aliwafundisha mataifa yote kumjua Mungu, akaziunganisha lugha mbalimbali za watu katika kuungama imani moja. Kwa sababu hiyo, katika upeo wa furaha ya kipasaka, ulimwengu mzima unashangilia. Lakini pia nguvu za mbinguni na majeshi ya Malaika wanaimba utenzi wa utukufu wako, wakisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu

ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.5:7-8
Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakasema matendo makuu ya Mungu, aleluya!

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu, unayelijalia Kanisa lako mapaji ya mbinguni, uilinde ndani yetu neema yako.Na kipaji cha Roho Mtakatifu ulichotumiminia kisitawi daima; nacho chakula cha kiroho kitufae kutuletea kwa wingi ukombozi wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

KUAGANA
K. Nendeni na amani ya Kristo, aleluya, aleluya.
W. Tumshukuru Mungu, aleluya, aleluya.