Generic placeholder image

JUMAPILI YA PENTEKOSTE
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina, aleluya.

UTENZI
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mliye sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.

ANT. I: Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu mzima, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu mzima, aleluya.

ANT. II: Utuletee nguvu yako, Bwana, kutoka hekalu lako takatifu lililoko Yerusalemu, na uikamilishe kazi yako kati yetu, aleluya.

Zab.114:1-8 Mungu pamoja na watu wake
Nanyi mliouacha ulimwengu huu, tambueni kuwa mmeokolewa kutoka Misri (Mt. Augustino)

Watu wa Israeli walipoondoka nchini Misri,*
wazao wa Yakobo walipotoka ugenini,

Yuda likawa taifa takatifu la Mungu,*
Israeli ikawa mali yake mwenyewe.

Bahari ya Shamu iliona ikakimbia;*
mto Yordani ukaacha kutiririka!

Milima ilirukaruka kama kondoo dume,*
vilima vikaruka kama wana-kondoo!

Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?*
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?

Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?*
Nanyi vilima, imekuwaje mkaruka kama wanakondoo?

Tetemeka, ewe dunia, mbele yake Mungu;*
Naam, mbele ya Mungu wa Yakobo,

anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,*
nayo majabali yakawa chemchemi za maji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Utuletee nguvu yako, Bwana, kutoka hekalu lako takatifu lililoko Yerusalemu, na uikamilishe kazi yako kati yetu, aleluya.

ANT. III: Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo
Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

Ant. III: Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema, aleluya.

SOMO: Ef.4:3-6
Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja; kuna Mungu mmoja na Baba wa wote ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote.

KIITIKIZANO
K. Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu mzima, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Yeye ndiye anayeviwezesha vitu vyote kuendelea kuwako, na ndiye anayeelewa kila neno lisemwalo.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Hii ndiyo siku ya Pentekoste, aleluya; leo Roho Mtakatifu aliwatokea mitume katika umbo la moto, na akawapatia vipaji vyake mahsusi; aliwatuma waende ulimwenguni, kutangaza kwamba ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Hii ndiyo siku ya Pentekoste, aleluya; leo Roho Mtakatifu aliwatokea mitume katika umbo la moto, na akawapatia vipaji vyake mahsusi; aliwatuma waende ulimwenguni, kutangaza kwamba ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka, aleluya.

MAOMBI
Tunajua kuwa Baba yu pamoja nasi kwa sababu ya Roho aliyetuletea. Kwa matumaini hayo tunakuelekea wewe, tukisali:
W. Baba, uliletee Kanisa Roho wako.

Baba, unataka kuwaunganisha watu wote kwa ubatizo katika Roho;
- uwaunganishe waamini wote katika akili na utashi. (W.)

Umemtuma Roho kuijaza dunia upendo wako;
- uwawezeshe binadamu kuunda jumuiya zao katika haki na amani. (W.)

Bwana Mungu, Baba wa watu wote, uwapatie umoja wa imani watoto wako waliotawanyika:
- uhuishe ulimwengu kwa nguvu ya Roho wako. (W.)

Kwa kazi ya Roho wako waziumba upya akili zote:
- uwaponye wagonjwa, uwafariji wanaodhulumiwa, na uwafikishe watu wote kwenye wokovu. (W.)

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, ulimfufua Mwanao kutoka wafu.
- Utufufue kwa nguvu ya Roho wako tutakapoufikia ufalme wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, unalitakatifuza Kanisa lako katika kila kabila na taifa kwa fumbo tunaloadhimisha leo. Uwapatie watu wote vipaji vya Roho Mtakatifu, na utimilize sasa katika mioyo ya waamini wako kile ambacho ulitekeleza wakati Injili ilipotangazwa kwa mara ya kwanza duniani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.

KUAGANA
K. Nendeni na amani ya Kristo, aleluya, aleluya.
W. Tumshukuru Mungu, aleluya, aleluya.