Generic placeholder image

JUMAPILI YA PENTEKOSTE
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Amani ya kweli tuipate;
Mfukuzie mbali mwuaji,
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mliye sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.

ANT. I: Siku ya Pentekoste wote walikuwa mahali pamoja, aleluya.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Siku ya Pentekoste wote walikuwa mahali pamoja, aleluya.

ANT. II: Vikatokea vitu vilivyoonekana kwa mitume kama ndimi za moto, na Roho Mtakatifu akamshukia kila mmoja wao, aleluya.

Zab.147:1-11 Ni vizuri kumsifu Mungu
Ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa;*
ni vizuri na sawa kabisa kumsifu.

Mungu anaurekebisha mji wa Yerusalemu.*
Anawarudisha salama wakimbizi wake.

Anawaponya waliovunjika moyo;*
anawatibu majeraha yao.

Ameiweka idadi ya nyota,*
na kuzipa kila moja jina.

Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi;*
maarifa yake hayana kipimo.

Mungu huwakweza wanyenyekevu,*
lakini huwatupa waovu mavumbini.

Mwimbieni Mungu nyimbo za shukrani,*
mpigieni kinubi Mungu wetu!

Yeye hulifunika anga kwa mawingu,/
huitengenezea dunia mvua,*
na kuchipusha nyasi vilimani.

Huwapa wanyama chakula chao,*
na kulisha makinda ya kunguru wanaolia.

Yeye hapendezwi na nguvu za farasi,*
wala hafarijiki kwa ushujaa wa askari;

lakini hupendezwa na watu wamchao,*
watu wanaotegemea upendo wake mkuu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Vikatokea vitu vilivyoonekana kwa mitume kama ndimi za moto, na Roho Mtakatifu akamshukia kila mmoja wao, aleluya.

ANT. III: Roho Mtakatifu, atokaye kwa Baba, atanitukuza, aleluya.

WIMBO: Ufu.15:3-4
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako?*
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Roho Mtakatifu, atokaye kwa Baba, atanitukuza, aleluya.

SOMO: Rom.8:11
Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu katika wafu anaishi ndani yenu, basi, huyo aliyemfufua Kristo katika wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa, atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Njoo, Roho Mtakatifu, uijaze mioyo ya waamini wako, na uwashe ndani yao moto wa upendo wako; ingawa wale watu walikuwa wa lugha tofauti, uliwaunganisha wote katika kuitangaza imani moja, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Njoo, Roho Mtakatifu, uijaze mioyo ya waamini wako, na uwashe ndani yao moto wa upendo wako; ingawa wale watu walikuwa wa lugha tofauti, uliwaunganisha wote katika kuitangaza imani moja, aleluya.

MAOMBI
Mitume walingojea, na kusali kwa ajili ya ujio wa Roho. Tukiwa tumekusanyika pamoja na kujiunga nao, tunasali jioni hii kwa ajili ya ujio wake kwetu, na kwa furaha tunatangaza ukuu wa Mungu.
W. Baba, utuletee Roho wako.

Katika Kristo uliutengeneza ulimwengu uliouumba;
- kwa njia ya Roho wako uipatie dunia imani mpya. (W.)

Ulimpulizia Adamu pumzi ya uzima:
- ulipulizie Kanisa Roho wako Mtakatifu, ili ulimwengu uweze kujipatia uzima katika Kanisa. (W.)

Roho wako alete mwanga kwenye giza letu;
- geuza chuki iwe upendo, huzuni iwe furaha, na mashaka yawe matumaini. (W.)

Utuoshe na kutuburudisha katika maji ya Roho:
- utuondolee uchungu na dhambi, kwa kutuponya na kutuwezesha kuzaliwa upya. (W.)

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, unawafikisha watu kwenye uzima na utukufu:
- uwawezeshe marehemu kuingia katika makao yao mbinguni, na kufurahia upendo wako milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, ulipanga hivi kwamba fumbo la Pasaka likamilishwe kwa fumbo la Pentekoste. Kwa neema yako, unganisha mataifa yaliyotawanyika na lugha zilizogawanyika katika imani moja, imani katika Jina lako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.