Generic placeholder image

JUMAPILI YA PENTEKOSTE
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Aleluya, Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu mzima. Njooni, tumwabudu, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Upepo mkali sana
Waja kasi duniani,
Una nguvu sana sana
Wavuma unakotoka:
Ndiye Roho wake Bwana,
Chemchemi ya ukweli,
Chanzo cha uhuru wote.

Roho ndiye bomba wazi
La kuyarushia maji
Milele juu mbinguni,
Maji yake yanaleta
Uhai usiokoma,
Chemchemi yake bora
Milele haikauki.

Roho aja kwa miali
Na ndimi za moto nyingi,
Na upendo na hekima
Aja navyo vinawaka,
Upepo, bomba na moto
Vyaungana vyote leo
Sikukuu ya mwangaza.

Ewe Roho mtulivu,
Utuletee amani,
Pamoja na Baba Mungu
Naye Mwana twakusifu,
Utatu Mtakatifu,
Kamwe usobadilika,
Milele Mungu Mmoja.

ANT. I: Bwana, jinsi Roho wako alivyo mwema na mkarimu ndani yetu! Aleluya.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Bwana, jinsi Roho wako alivyo mwema na mkarimu ndani yetu! Aleluya.

ANT. II: Kila chemchemi ya maji na imtukuze Bwana; kila kitu kinachoishi majini na kimwimbie Mungu utenzi, aleluya.

WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

ANT. II: Kila chemchemi ya maji na imtukuze Bwana; kila kitu kinachoishi majini na kimwimbie Mungu utenzi, aleluya.

ANT. III: Mitume walisema kwa lugha mbalimbali, na kutangaza matendo ya ajabu ya Mungu, aleluya.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mitume walisema kwa lugha mbalimbali, na kutangaza matendo ya ajabu ya Mungu, aleluya.

SOMO: Mate.5:30-32
Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani. Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa Kiongozi na Mkombozi, ili awawezeshe watu wa Israeli kutubu, wapate kusamehewa dhambi zao. Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo.

KIITIKIZANO
K. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Wakaanza kusema.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wote...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Pokeeni Roho Mtakatifu. Wote mtakaowaondolea dhambi zao, watasamehewa, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Pokeeni Roho Mtakatifu. Wote mtakaowaondolea dhambi zao, watasamehewa, aleluya.

MAOMBI
Siku hii ya Pentekoste, Kanisa limejaa furaha. Tukiwa tumeimarishwa kwa matumaini yasiyo na kipimo, tunamwomba Kristo, anayewaita waamini Wake wakusanyike pamoja katika Roho Mtakatifu.
W. Bwana, uufanye upya uso wa dunia.

Bwana Yesu, ukiwa umesulibiwa msalabani, ulimwaga maji ya ubatizo kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
- Uyatie chachu maisha ya binadamu wote, kwa njia ya Roho Mtakatifu. (W.)

Baada ya kutukuzwa kuumeni kwa Mungu, uliwapatia mitume wako Zawadi itokayo kwa Baba;
- Kanisa lako sasa linangoja kupata Zawadi hiyo hiyo, tumaini hilo hilo. (W.)

Uliwapulizia mitume Roho wako, na kuwapatia uwezo wa kusamehe:
- uwafungulie na kuwatoa watu wote leo katika jela ya dhambi. (W.)

Uliahidi kutuletea Roho wako wa ukweli, ili tuweze kuwa wajumbe wako ulimwenguni kote.
- Kwa uwepo wake katika Kanisa, tuweze kukushuhudia wewe kiaminifu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, unalitakatifuza Kanisa lako katika kila kabila na taifa kwa fumbo tunaloadhimisha leo. Uwapatie watu wote vipaji vya Roho Mtakatifu, na utimilize sasa katika mioyo ya waamini wako kile ambacho ulitekeleza wakati Injili ilipotangazwa kwa mara ya kwanza duniani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.