MWILI NA DAMU YA KRISTO MWAKA C MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.81:16
Nimewalisha kwa unono wa ngano, nimewashibisha kwa asali itokayo mwambani.
Utukufu husemwa.
KOLEKTA:
Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika sakramenti ya ajabu. Tunakuomba utujalie
kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya Mwili na Damu yako, tupate kuona daima ndani yetu tunda la
ukombozi wako. Unayeishi na kutawala pamoja na Mungu Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu,
milele na milele.
SOMO 1: Mwa.14:18-20
Melkizedeki mfalme wa Salemu alileta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.
Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe
Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.110:1-4 (K)4
1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako
Kuwa chini ya miguu yako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.
2. Bwana atainyosha toka Sayuni
Fimbo ya nguvu zako,
Uwe na enzi kati ya adui zako. (K)
3. Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi,
Unao umande wa ujana wako. (K)
4. Bwana ameapa,
Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)
SOMO 2: 1Kor.11:23-26
Mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,
naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi
kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema. Kikombe hiki ni agano
jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate
huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
SHANGILIO: Yn.6:51
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi chakula chenye uzima
kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana;
mtu akila chakula hiki, ataishi milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:11-17
Makutano walipojua walimfuata Yesu akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu,
akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara,
wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa
kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu. Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema,
Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote
vyakula. Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni
watu kwa safu, kila safu watu hamsini. Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Akaitwaa ile mikate
mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akivibariki, akavimega, akawapa wanafunzi
wake ili wawaandikie mkutano. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyobakia walikusanya
vikapu kumi na viwili.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu waumini, Yesu hakuwaaga wasikilizaji wake bila kuwapa chakula. Aliongeza mikate na samaki
ili kulisha umati. Kwa njia hiyo anatukumbusha kwamba ni wajibu wetu wa kuwalisha wenye shida.
Ee Bwana Yesu,
1. Uliwalisha watu jangwvani, utusaidie kutafuta njia za kuwalisha wale wote wenye njaa.
2. Ulitangaza mambo ya kiroho, lakini ulijali vile vile mahitaji ya mwili. Utuangaze tusiwasahau
wenzetu wenye shida za mwili na za roho.
3. Utujalie roho ya ukarimu. Utuhimize tusiwanyime msaada wetu wale wote wasiojiweza.
4. Kugawa chakula kunawaunganisha wote, watoaji na wapokeaji katika umoja wa pekee: Utusaidie
kukomesha roho ya uchoyo.
Ee Mungu Baba. Mwana wako alituachia karamu ya Ekaristi ili ituunganishe katika umoja wa maisha
na imani. Utusaidie kushinda sababu zote za utengano kati yetu kwa nguvu ya karamu aliyotuwekea
Bwana wetu Yesu Kristo anayeishi na kutawala pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, daima
na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kulijalia Kanisa lako umoja na amani, ambavyo huoneshwa kwa
fumbo chini ya maumbo ya vipaji tunavyokutolea. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.6:56
Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunaomba utujalie tuufurahie kikamilifu uzima wako wa kimungu katika karamu ya milele,
ambao umetuonjesha katika kupokea Mwili na Damu yako azizi hapa duniani. Unayeishi na kutawala
milele na milele.