MOYO MTAKATIFU WA YESU MWAKA C MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.33:11,19
Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi, yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka fadhili za ajabu za mapendo yake kwetu. Tunakuomba utujalie tustahili kupokea neema tele katika chemchemi hiyo ya karama za mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

Au:
Ee Mungu, kwa huruma yako unapenda kutujalia hazina isiyopimika ya upendo katika Moyo wa Mwanao uliojeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu. Tunakuomba utujalie ili, kwa kumtolea heshima ya ibada yetu, tutimize pia wajibu wa malipizi yatupasayo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Eze.34:11-16
Bwana Mungu asema hivi: Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, na juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu nami nitawalaza, asema Bwana Mungu. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.23, (K)1
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu;
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu
Sitapungukiwa na kitu.

2. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kiombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

SOMO 2: Rum.5:5-11
Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki, lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Basi Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na gadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumepokea huo upatanisho.

SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi mchungaji mwema;
asema Bwana;
nao walio wangu nawajua;
na walio wangu wanijua mimi;
Aleluya!

INJILI: Lk.15:3-7
Yesu aliwaambia mfano huu, ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aenda akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, Bwana Yesu alijionesha kwetu kama mchungaji mwema anayeacha kondoo tisini na tisa jangwani ili kumtafuta mmoja aliyepotea.

Ee Bwana Yesu,
1. Ulifanya juu chini ili kumpata kondoo mmoja aliyepotea. Utupe matumaini ya kutokuachwa katika shida na utuokoe katika kila hatari.

2. Wewe ulisema kwamba ni mchungaji mwema. Utuzibue masikio yetu ili tusikie sauti yako na kukufuata kama kiongozi katika njia ya kwenda kwa Baba.

3. Unafurahi kuwakaribisha waliopotea na kukurudia. Usituache katika hali ya kukusahau, bali utuhimize kurudi kwako uliye chemchemi ya furaha yetu.

4. Wewe ni mchungaji unayehatarisha maisha yako kwa ajili yetu. Utuwezeshe kukutumaini na kukutegemea daima.

Ee Mungu Baba, Mwana wako alijibidisha sana kutuokoa hata kutoa maisha yake. Ana nia ya kutuchunga tusipotee katika njia ya kufika kwako. Tunaomba hayo kwa njia yake yeye anayeishi na kutawala nawe milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utazame upendo usio na kifani wa Mwanao mpenzi, ili sadaka tunayokutolea ikupendeze na kuwa kwetu fidia ya dhambi zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Mapendo Makuu ya Kristo.
K.
Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye aliinuliwa msalabani, akajitoa mwenyewe kwa upendo wa ajabu kwa ajili yetu. Alichomwa ubavu, akamwaga damu na maji, zipate kububujika kutoka humo sakramenti za Kanisa, ili wote wavutwe na huo Moyo wazi wa Mwokozi, na kuchota siku zote kwa furaha neema katika chemchemi hiyo ya wokovu.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Watakatifu na Malaika wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.7:37-38
Bwana asema: Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

Au: Yn.19:34
Askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti hii ya mapendo ituwashie upendo mtakatifu, ambao, kwa kutuvutia daima kwa Mwanao, utufundishe kumtambua yeye katika ndugu zetu. Anayeishi na kutawala milele na milele.