KUPAA BWANA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Mdo.1:11
Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Yesu atakuja jinsi hiyohiyo mlivyomwona
akienda zake mbinguni, aleluya!
Utukufu husemwa.
KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi, utufanye tufurahi kwa furaha takatifu, na kuchangamka kwa tendo la ibada ya
shukrani, kwani kupaa kwake Kristo Mwanao ni kuinuliwa kwetu; na kule alikotutangulia yeye kichwa
chetu, kwa utukufu, hukohuko twatumaini kuweko pia sisi mwili wake. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
Au:
Ee Mungu mwenyezi, sisi tunasadiki kwamba leo Mwanao pekee Mkombozi wetu amepaa mbinguni.
Tunakuomba utujalie nasi pia tuwe tunaishi mbinguni kiroho. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na
milele.
SOMO 1: Mdo.1:1-11
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu
kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa
Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi,
baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo
yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali
waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji,
bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika,
wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia,
Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo,
walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho
mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,
wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka
kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.47:1-2,5-6,7-8(K)5
1. Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Au:
Aleluya.
2. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
3. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
SOMO 2: Efe.1:17-23
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika
kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri
wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu
tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo
alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko
ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu
tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya
vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote
katika vyote.
SHANGILIO: Mt.28:19-20
Aleluya, aleluya!
Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote
Aleluya!
INJILI: Lk.24:46-53
Yesu aliwaambia wafuasi wake, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya
tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi,
kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na, tazama, nawaletea juu yenu
ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka
Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa
juu mbinguni. Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani
ya hekalu, wakimsifu Mungu.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ee Bwana Yesu Kristo, ulipotuma mitume kueneza habari ya wokovu uliwaahidia msaada wa Roho
Mtakatifu.
Ee Bwana Yesu,
1. Ulikubali kufa kwa ajili yetu ili sisi tukombolewe. Utuoneshe njia ya kuwatangazia wote
furaha ya ukombozi wetu.
2. Kufa kwako kulituletea ondoleo la dhambi na kutupa mwanzo mpya wa maisha. Utusaidie kushuhudia
maisha hayo mapya kila siku katika kupatana na wenzetu.
3. Bila msaada kutoka juu tunashindwa kuishi kadiri ya matakwa ya wokovu. Utupe nguvu ya Roho Mtakatifu
atusaidie katika maisha yetu ya kila siku.
4. Mitume walitumwa waende duniani kote. Utupe nguvu ya Roho Mtakatifu ili atusaidie kukushuhudia
kwa watu tunaoishi nao.
5. Kwa kupaa mbinguni ulitupa matumaini makubwa ya kukufuata katika utukufu wako wa milele. Utujaze
furaha ya kukaribishwa kwako mbinguni baada ya maisha magumu ya duniani.
Ee Mungu Baba, Mwana wako alituonesha njia ya kufika kwako na kurithi uzima wako wa milele. Alitutangulia
ili kututayarishia makao ya baadaye. Usikilize maombi yetu kwa njia yake yeye aliyetutangulia mbinguni.
Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakutolea kwa unyenyekevu sadaka hii, kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba
utujalie ili, kwa njia ya mabadilishano haya matakatifu ya vipaji, tupate kuinuliwa hadi mambo ya
mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.28:20
Tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari, aleluya!
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi wa milele, wewe unatujalia tuliopo hapa duniani tuweze kuyashughulikia mambo
ya mbinguni. Tunakuomba uuelekeze moyo wa ibada Wa sisi wakristo huko aliko Bwana Yesu, aliyechukua
ubinadamu wetu. Anayeishi na kutawala milele na milele.