KUPAA BWANA MWAKA A
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Mdo.1:11
Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Yesu atakuja jinsi hiyohiyo mlivyomwona
akienda zake mbinguni, aleluya!
Utukufu husemwa.
KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi, utufanye tufurahi kwa furaha takatifu, na kuchangamka kwa tendo la ibada ya
shukrani, kwani kupaa kwake Kristo Mwanao ni kuinuliwa kwetu; na kule alikotutangulia yeye kichwa
chetu, kwa utukufu, hukohuko twatumaini kuweko pia sisi mwili wake. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
Au:
Ee Mungu mwenyezi, sisi tunasadiki kwamba leo Mwanao pekee Mkombozi wetu amepaa mbinguni.
Tunakuomba utujalie nasi pia tuwe tunaishi mbinguni kiroho. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na
milele.
SOMO 1: Mdo.1:1-11
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu
kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa
Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi,
baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo
yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali
waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji,
bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika,
wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia,
Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo,
walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho
mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,
wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka
kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.47:1-2,5-6,7-8(K)5
1. Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Au:
Aleluya.
2. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
3. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
SOMO 2: Efe.1:17-23
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika
kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri
wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu
tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo
alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko
ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu
tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya
vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote
katika vyote.
SHANGILIO: Mt.28:19-20
Aleluya, aleluya!
Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote
Aleluya!
INJILI: Mt.28:16-20
Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona,
walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa
mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza
kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Baada ya ufufuko wake, Yesu aliwatokea wafuasi wake mara kwa mara. Lakini siku moja aliwatokea
kwa mara ya mwisho. Alipaa mbinguni kututangulia sisi sote ili kututayarishia makao ya milele
mbinguni. Kabla ya kupaa Yesu aliwapa mitume maagizo ya kuendeleza ujumbe wake wa kueneza habari
ya wokovu kwa watu wote.
Ee Bwana Yesu,
1. Ulitimiza wokovu kwa wote, kwa hiyo uliweza kusema kwamba umekabidhiwa mamlaka yote mbinguni
na duniani. Utujalie kuonja na kufurahia mamlaka yako katika maisha yetu.
2. Uliwaagiza mitume wako kwenda duniani kote ili kutangaza habari ya wokovu. Utupe moyo wa kuishi
kadiri ya wokovu tuliojaliwa.
3. Uliwaagiza mitume wako wafundishe watu wote amri zako. Utusaidie kuzishika amri zako ili kuwaonesha
wote kwamba juu ya msingi wa amri zako ni msingi wa mafanikio ya maisha.
4. Uliwaagiza mitume wako kuwabatiza watu. Utusaidie kwa njia ya matendo yetu kuwavuta watu wengine
wajiunge na jamii ya waumini.
5. Ulituahidia kuwa nasi mpaka mwisho wa dunia. Utuoneshe enzi na msaada wako katika matatizo yetu
ya kila siku.
Ee Bwana Yesu, siku ya mwisho utakuja tena kwa utukufu wako. Roho Mtakatifu atupe nguvu ya kupigania
imani na kuitunza. Kwa njia hiyo tujaliwe taji la uzima wa milele ambao ulituahidia wewe unayeishi
na kutawala pamoja na Mungu Baba daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakutolea kwa unyenyekevu sadaka hii, kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba
utujalie ili, kwa njia ya mabadilishano haya matakatifu ya vipaji, tupate kuinuliwa hadi mambo ya
mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.28:20
Tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari, aleluya!
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi wa milele, wewe unatujalia tuliopo hapa duniani tuweze kuyashughulikia mambo
ya mbinguni. Tunakuomba uuelekeze moyo wa ibada Wa sisi wakristo huko aliko Bwana Yesu, aliyechukua
ubinadamu wetu. Anayeishi na kutawala milele na milele.