SHEREHE YA KUPAA BWANA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Bwana Mungu, enzi yako yatukuzwa juu ya mbingu, aleluya.
Adhuhuri
Ant.: Huchomoza upande huu wa mbingu, na safari yake huishia kwenye
upeo wa mbingu, aleluya.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Aliinua mikono yake juu, akawabariki. Na alipokuwa anawabariki,
akachukuliwa mbinguni, aleluya.
Zab.8 Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa Kanisa, akiwa ndio
mkuu wa vitu vyote (Ef.1:22)
Ee Mwenyezi, Bwana wetu,/
jina lako latukuka kote duniani!*
Utukufu wako wafika hata mbinguni;
wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wachanga/
Wewe uko imara mbele ya wapinzani wako;*
wawakomesha maadui na waasi.
Nikiangalia anga,/
kazi ya vidole vyako mwenyewe,*
mwezi na nyota ulivyoviumba:
mtu ni nini, Ee Mungu, hata umfikirie?*
Mwanadamu ni nini hata umjali?
Hata hivyo, ulimfanya mdogo kidogo tu,/
kuliko wewe mwenyewe,*
na umemvika taji ya utukufu na heshima.
Ulimpa mamlaka juu ya kazi zako zote;*
uliviweka viumbe vyote chini ya miguu yake:
kondoo, ng'ombe na wanyama wa porini;*
ndege, samaki na viumbe vyote vya baharini.
Ee Mwenyezi, Bwana wetu:*
Jina lako latukuka duniani kote!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.19A Utukufu wa Mungu katika viumbe
Mwanga utokao juu umetufikia kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani (Lk.1:79)
Mbingu zadhihirisha utukufu wa Mungu;*
anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana waupasha habari mchana ufuatao,*
usiku waufahamisha usiku ufuatao.
Hamna msemo au maneno yanayotumika;*
wala hakuna sauti inayosikika;
hata hivyo, sauti yao yaenea nchini kote;*
ujumbe wao wasikika popote duniani.
Mungu ameliwekea jua makao yake angani;/
nalo latoka nje kama bwana arusi,*
kama shujaa aliye tayari kushindana.
Lachomoza toka upande mmoja,/
na kuzunguka hadi upande mwingine;*
wala hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.19B:7-14. Sheria ya Mungu
Basi, mwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu (Mt.5:48)
Sheria ya Mungu ni kamilifu,*
humrudishia mtu nguvu;
agizo la Mungu ni thabiti,*
huwapa hekima wasio na makuu.
Amri za Mungu ni sawa,*
hufurahisha moyo;
agizo la Mungu ni la haki,*
humwelimisha mtu.
Kumcha Mungu ni jambo jema,*
uchaji wa Mungu wadumu milele;
hukumu za Mungu ni sawa,*
zote nizahaki kabisa.
Zatamanika kuliko dhahabu;*
kulikodhahabu safi kabisa.
Ni tamu kuliko asali;*
kuliko asali safi kabisa.
Zanifunza mimi mtumishi wako;*
kuzitii kwaniletea tuzo kubwa.
Lakini nani ayaonaye makosa yake mwenyewe?*
Ee Mungu, niepushe na makosa yale nisiyoyajua.
Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi,*
usikubali hayo yanitawale.
Hapo nitakuwa mkamilifu;*
sitakuwa na dhambi kubwa.
Maneno na mawazo yangu yakupendeze, Ee Mungu,*
mwamba wa usalama wangu na mkombozi wangu!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Bwana Mungu, enzi yako yatukuzwa juu ya mbingu, aleluya.
Adhuhuri
Ant.: Huchomoza upande huu wa mbingu, na safari yake huishia kwenye
upeo wa mbingu, aleluya.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Aliinua mikono yake juu, akawabariki. Na alipokuwa anawabariki,
akachukuliwa mbinguni, aleluya.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Uf.1:17c-18
Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini,
tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninayo mamlaka juu ya kifo na kuzimu.
K. Msifadhaike mioyoni mwenu, aleluya.
W. Naenda kwa Baba yangu, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Ufu.1:17c-18
Sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha
Mwenyezi Mungu mbinguni. Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika mahali Patakatifu sana,
yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, Sio na binadamu. Kila Kuhani Mkuu
ameteuliwa kumtolea Mungu zawadi na sadaka.
K. Bwana alimtayarishia kiti cha enzi, aleluya.
W. Alimwanzishia utawala wake mbinguni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:1-2
Basi, ikiwa mmekufa pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, amekaa upande
wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani.
K. Msifuni Mfalme wa wafalme, aleluya.
W. Mwimbieni Mungu utenzi, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, utujaze furaha takatifu, utufundishe jinsi ya kukushukuru kwa heshima
na mapendo kwa ajili ya kupaa kwa Kristo Mwanao. Umetufufua pamoja naye: huko ambako yeye,
kichwa chetu, ametutangulia kwa utukufu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.