Generic placeholder image

SHEREHE YA KUPAA BWANA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele Amina, aleluya.

UTENZI
Bwana mbinguni apaa
Kwa makelele ya shangwe,
Tarumbeta zatangaza
Ushindi wake mkuu;
Pamoja naye wapaa
Utu na ubinadamu
Ili ukakae juu
Kupita kwa malaika.

Amekaa naye Mungu
Mkonowe wa kulia,
Mungu ambaye ni Bwana
Mkubwa wa kila kitu;
Utukufu wake Baba
Ni pia wake mwenyewe:
Kristo Yesu Bwana,
Mfalme wa viumbe vyote.

Atakapokuja tena
Kwa enzi na utukufu
Na sote kutufufua
Siku hiyo maarufu,
Tutakusanywa pamoja
Tusimame mbele yake,
Kila chozi litafutwa
Tutafurahia sote.

Ee Mungu, Baba yetu,
Isikie yetu sala:
Na Kristo, Bwana wetu,
Wa pekee wako Mwana,
Umtume Roho kwetu,
Roho wa upendo wako,
Aje kaa ndani mwetu
Na kutufanya mmoja.

ANT. I: Alipaa mbinguni; ameketi mkono wa kuume wa Baba, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Alipaa mbinguni; ameketi mkono wa kuume wa Baba, aleluya.

ANT. II: Mungu anapaa kwa kelele za shangwe; Bwana anapanda juu kwa mlio wa tarumbeta, aleluya.

Zab.47 Utawala Mkuu
Enyi watu wote, pigeni makofi!*
Msifuni Mungu kwa shangwe!

Maana Mungu, Mungu Mkuu, anatisha.*
Ni mfalme mkuu wa ulimwengu wote.

Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa,*
ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.

Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu,*
ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.

Mungu amepanda juu huku akishangiliwa,/
Mungu amepanda juu akipigiwa tarumbeta.

Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni!*
Mwimbieni Mfalme wetu sifa, mwimbieni!

Mungu ni mfalme wa ulimwengu wote;*
mwimbieni sifa kwa tenzi.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
“Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.“

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mungu anapaa kwa kelele za shangwe; Bwana anapanda juu kwa mlio wa tarumbeta, aleluya.

ANT. III: Sasa mwana wa Mtu ametukuzwa, na katika yeye Mungu ametukuzwa, aleluya.

WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-1
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!

Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!

Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.

Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,

watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.

Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!

Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu

akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.

Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwanakondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;

maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.

Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Sasa mwana wa Mtu ametukuzwa, na katika yeye Mungu ametukuzwa, aleluya.

SOMO: 1Pet.3:18,22
Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke ninyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili, lakini akafanywa hai kiroho; ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.

KIITIKIZANO
K. Ninapaa kwenda kwa Baba yangu na Baba yenu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Naenda kwa Mungu wangu na Mungu wenu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ninapaa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mfalme wa Utukufu, Bwana Mwenyezi, leo umepaa mbinguni kwa ushindi: usituache kama yatima wasio na mlezi, bali umtume kwetu yule uliyetuahidi, zawadi itokayo kwa Baba, Roho wa Ukweli, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mfalme wa Utukufu, Bwana Mwenyezi, leo umepaa mbinguni kwa ushindi: usituache kama yatima wasio na mlezi, bali umtume kwetu yule uliyetuahidi, zawadi itokayo kwa Baba, Roho wa Ukweli, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Bwana ambaye sasa ameinuliwa juu kutoka duniani, akavivutia kwake vitu vyote.
W. Wewe, Kristo, ndiwe mfalme wa utukufu.

Bwana Yesu, ulitolea sadaka moja kwa ajili ya dhambi, na halafu ukapaa kwa ushindi kwenda kwa Baba;
- uwawezeshe wale unaowatakatifuza kupata ukamilifu wao wa milele. (W.)

Kuhani wa milele, mhudumu wa agano jipya, wewe u hai na unatuombea;
- uwaokoe watu wako wanaokuelekea na kukuomba. (W.)

Baada ya mateso yako uliwatokea wanafunzi wako, nao walitambua kwamba u hai:
- utusadikishe tuamini kuwa wewe upo nasi leo. (W.)

Siku ya leo uliwaahidi mitume kwamba wangepata Roho Mtakatifu, ili waweze kueneza injili yako mpaka miisho ya dunia;
- utuimarishe kwa nguvu ya Roho Mtakatifu katika kukushuhudia wewe ulimwenguni. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi, utujaze furaha takatifu, utufundishe jinsi ya kukushukuru kwa heshima na mapendo kwa ajili ya kupaa kwa Kristo Mwanao. Umetufufua pamoja naye: huko ambako yeye, kichwa chetu, ametutangulia kwa utukufu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.