SHEREHE YA KUPAA BWANA
MASIFU YA JIONI I
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Bwana mbinguni apaa
Kwa makelele ya shangwe,
Tarumbeta zatangaza
Ushindi wake mkuu;
Pamoja naye wapaa
Utu na ubinadamu
Ili ukakae juu
Kupita kwa malaika.
Amekaa naye Mungu
Mkonowe wa kulia,
Mungu ambaye ni Bwana
Mkubwa wa kila kitu;
Utukufu wake Baba
Ni pia wake mwenyewe:
Kristo Yesu Bwana,
Mfalme wa viumbe vyote.
Atakapokuja tena
Kwa enzi na utukufu
Na sote kutufufua
Siku hiyo maarufu,
Tutakusanywa pamoja
Tusimame mbele yake,
Kila chozi litafutwa
Tutafurahia sote.
Ee Mungu, Baba yetu,
Isikie yetu sala:
Na Kristo, Bwana wetu,
Wa pekee wako Mwana,
Umtume Roho kwetu,
Roho wa upendo wako,
Aje kaa ndani mwetu
Na kutufanya mmoja.
ANT. I: Nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa naondoka
ulimwenguni, ili niende kwa Baba, aleluya.
Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!
Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.
Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!
Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.
Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;
lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.
Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,
na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.
Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa naondoka
ulimwenguni, ili niende kwa Baba, aleluya.
ANT. II: Alipokwisha sema na wanafunzi wake, Bwana Yesu alipaa
mbinguni, ambako ameketi kuume kwa Baba, aleluya.
Zab.117 Kumsifu Mungu
Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!
Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Alipokwisha sema na wanafunzi wake, Bwana Yesu alipaa
mbinguni, ambako ameketi kuume kwa Baba, aleluya.
ANT. III: Hapana yeyote aliyepaa mbinguni, isipokuwa yeye aliyeshuka
kwanza kutoka mbinguni, Mwana wa Mtu, ambaye yuko mbinguni, aleluya.
WIMBO: Ufu.11:17-18;12:10b-12a
Bwana Mungu Mwenyezi,*
uliyeko na uliyekuwako!
Tunakushukuru,/
maana umetumia nguvu yako kuu*
ukaanza kutawala!
Watu wa mataifa waliwaka hasira,/
maana wakati wa ghadhabu yako umefika,*
wakati wa kuwahukumu wafu.
Ndio wakati wa kuwatuza*
watumishi wako manabii,
watu wako na wote wanaolitukuza jina lako,*
wakubwa kwa wadogo.
Sasa wokovu utokao kwa Mungu umefika!/
Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika.*
Na Masiha wake ameonesha mamlaka yake!
Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu,*
aliyesimama mbele ya Mungu
akiwashtaki usiku na mchana,*
sasa ametupwa nje.
Ndugu zetu wameshinda/
kwa damu ya Mwana-kondoo*
na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza;
maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,*
wakawa tayari kufa.
Kwa sababu hiyo furahini enyi mbingu*
na vyote vilivyomo ndani yenu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Hapana yeyote aliyepaa mbinguni, isipokuwa yeye aliyeshuka
kwanza kutoka mbinguni, Mwana wa Mtu, ambaye yuko mbinguni, aleluya.
SOMO: Ef.2:4-6
Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata, ingawa tulikuwa
tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi
mmeokolewa. Kwa kuungana na Kristo Yesu Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye
mbinguni.
KIITIKIZANO
K. Mungu anapaa kwa kelele za shangwe, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Bwana anapanda juu kwa mlio wa tarumbeta.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mungu...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Baba, nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa; sasa nawaombea hao, siuombei ulimwengu,
kwa kuwa naja kwako, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Baba, nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa; sasa nawaombea
hao, siuombei ulimwengu, kwa kuwa naja kwako, aleluya.
MAOMBI
Kwa furaha, tumwombe Kristo ambaye ameketi mkono wa kuume wa Baba.
W. Wewe, Kristo, ndiwe mfalme wa utukufu.
Mfalme wa utukufu, katika wewe miili yetu ya kibinadamu imekwezwa juu kabisa;
- utuopoe kutoka katika uharibifu wa dhambi, na uturudishie uzima wa milele. (W.)
Kwa kufuata njia ya upendo, ulishuka kwetu kutoka mbinguni.
- utuwezeshe kufuata njia hiyo hiyo tunapopanda kukujia wewe. (W.)
Uliahidi kuwavutia watu wote kwako;
- usiruhusu hata mmoja wetu atengane na mwili wako. (W.)
Umepaa mbinguni;
- utuwezeshe kuwa huko pamoja nawe kwa mawazo na mioyo yetu. ((W.)
Tunangojea kukuona ukija kwa enzi siku hiyo ya hukumu;
- utujalie tuweze kuuangalia siku hiyo utukufu wako, pamoja na waamini wote marehemu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, utujaze furaha takatifu, utufundishe jinsi ya kukushukuru kwa heshima na
mapendo kwa ajili ya kupaa kwa Kristo Mwanao. Umetufufua pamoja naye: huko ambako yeye,
kichwa chetu, ametutangulia kwa utukufu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.
Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.