SHEREHE YA KUPAA BWANA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Aleluya, Kristo apaa mbinguni akiwa na hadhi ya Bwana. Njooni, tumwabudu, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI
Ewe mpanzi na mbegu
Ya wokovu wao watu,
Yesu raha tamaniwa
Ewe ya moyo faraja,
Umeondoa hatia
Kosa la viumbe vyako,
Nuru safi aijua
Aliye mpenzi wako;
Hiyo ni huruma gani
Kakuleta duniani,
Mzigo wetu wa dhambi
Ukatwikia kichwani,
Ukachinjwa ili eti
Taifa lilokuchinja
Lijipatie uzima
Kwa kifo ha kuonewa?
Kuzimu sasa ni fujo
Umekatwa mnyororo
Ule wa zama za zama,
Wafungwa ni huru sasa;
Wasongwa na roho hizo
Wafufuka u mzima,
Kuume kwa Baba yako
Sasa watawala Bwana.
ANT. I: Enyi wananchi wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama angani?
Yesu huyo ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kupelekwa mbinguni, atakuja tena namna hiyo hiyo
mlivyomwona akienda mbinguni, aleluya.
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Enyi wananchi wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama angani?
Yesu huyo ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kupelekwa mbinguni, atakuja tena namna hiyo hiyo
mlivyomwona akienda mbinguni, aleluya.
ANT. II: Mtukuzeni mfalme wa wafalme; msifuni Mungu, aleluya.
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Ant. II: Mtukuzeni mfalme wa wafalme; msifuni Mungu, aleluya.
ANT. III: Walipokuwa wanamtazama, alichukuliwa juu mbinguni, na
wingu likamficha wasimwone tena, aleluya.
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Walipokuwa wanamtazama, alichukuliwa juu mbinguni, na
wingu likamficha wasimwone tena, aleluya.
SOMO: Ebr.10:12-14
Kristo alitoa sadaka moja kwa ajili ya dhambi, sadaka ifaayo milele, kisha, akaketi upande
wa kulia wa Mungu. Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
Basi, kwa sadaka yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
KIITIKIZANO
K. Kristo alipaa juu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Akauteka nyara utumwa.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Ninapaa kwenda kwa Baba yangu na Baba yenu, Kwa Mungu wangu na Mungu wenu, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Ninapaa kwenda kwa Baba yangu na Baba yenu, Kwa Mungu wangu na
Mungu wenu, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Bwana ambaye sasa ameinuliwa juu kutoka duniani, akivivutia kwake vitu vyote.
W. Wewe Kristo, ndiwe mfalme wa utukufu.
Bwana Yesu, ulitolea sadaka moja kwa ajili ya dhambi, na halafu ukapaa kwa ushindi kwenda kwa Baba;
- uwawezeshe wale unaowatakatifuza kupata ukamilifu wao milele. (W.)
Kuhani wa milele, mhudumu wa agano jipya, wewe u hai na unatuombea;
- uwaokoe watu wako wanaokuelekea na kukuomba. (W.)
Baada ya mateso yako uliwatokea wanafunzi wako, nao walitambua kwamba u hai:
- utusadikishe tuamini kuwa wewe upo nasi leo. (W.)
Siku ya leo uliwaahidi mitume kwamba wangepata Roho Mtakatifu, ili waweze kueneza injili yako
mpaka miisho ya dunia;
- utuimarishe kwa nguvu ya Roho Mtakatifu katika kukushuhudia wewe ulimwenguni. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, utujaze furaha takatifu, utufundishe jinsi ya kukushukuru kwa heshima na
mapendo kwa ajili ya kupaa kwa Kristo Mwanao. Umetufufua pamoja naye: huko ambako yeye,
kichwa chetu, ametutangulia kwa utukufu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.
Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.