JUMATATU OKTAVA YA PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.2:14,22-32
Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa
Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo, mkasikilize maneno yangu. Enyi waume
wa Israeli, sikilizeni maneno haya; Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa
miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi
wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake
tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua,
akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari
zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume,
nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; tena mwili wangu nao
utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa Mtakatifu
wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; utanijaza furaha kwa uso wako. Waume, ndugu
zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa
alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa
Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti
chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo,
ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu
alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:1-2,5,7-11
1. Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
(K) Mungu unihifadhi mimi,
kwa maana nakukimbilia wewe.
Au:
Aleluya.
2. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)
3. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu.
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
4. Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele. (K)
SHANGILIO: Zab.118:24
Aleluya, aleluya,
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
tutaishangilia na kuifurahia.
Aleluya.
INJILI: Mt.28:8-15
Wanawake waliondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha
wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika
miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende
Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia
mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na
wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi
wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali,
sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama
walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.
MAOMBI
Ndugu zangu, Mungu hakutaka roho ya Mwanae iachwe kuzimu wala mwili wake uone uharibifu. Tunaposherehekea
ufufuko wake Kristo, tumwombe. Ee Mungu twakuomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uzidi kumdhihirisha kwetu Mwanao Mfufuka kwa miujiza, maajabu na ishara anazozifanya kwa mkono wako.
2. Uwaite vijana wengi kufanya kazi ya unabii na kumshuhudia Mwanao aliyeketi katika kiti chako cha enzi.
3. Utuepushe na hongo au tabia ya kutetea maslahi yetu kinyume na ukweli wako.
4. Uwafufue marehemu wetu na kuwafungulia uchungu wa mauti, ili roho na miili yao visionje uharibifu.
Ee Bwana Mungu, umependa wanawake waliomlilia Mwanao siku ya Ijumaa Kuu wawe mashahidi wa ufufuko wake; nao
wanamshika miguu na kumsujudia. Utupe nasi bidii ya kukupenda kwa moyo wote. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.