JUMATATU JUMA KUU
MASOMO
SOMO 1: Isa.42:1-7
Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia
roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya
isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima;
atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani;
na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda;
yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye
roho wao waendao ndani yake. Mimi, Bwana nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda,
na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa,
kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1-3, 13-14(K)1
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
2. Watenda mabaya waliponikaribia,
Wanile nyama yangu,
Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. (K)
3. Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata japo nitatumaini. (K)
4. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SHANGILIO: Eze.18:31
Tupilieni mbali nanyi
makosa yenu yote mliyoyakosa, asema Bwana,
jifanyieni moyo mpya na roho mpya.
INJILI: Yn.12:1-11
Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua
katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumika; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa
wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye
thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu
ya marhamu. Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema,
Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa
kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa
humo. Basi yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku za maziko yangu. Kwa maana maskini mnao siku zote
pamoja nanyi; bali mimi hamnami siku zote. Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa
yeye yuko huko; nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua
katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi
katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.
MAOMBI
Ee Mungu uliyeziumba mbingu na kuitandaza nchi na mazao yake, ndiwe unayewapa pumzi na roho watu walio juu
ya hiyo nchi. Kwa hiyo twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwatazame kwa wema Baba Mtakatifu F. na Askofu wetu F.
na watumishi wako wote uliowateua rasmi kwa ajili ya kuiendeleza kazi aliyoianzisha Mwanao.
2. Uwaimarishe wote wanaodhulumiwa kwa ajili ya jina lako, ili wayavumilie mateso na kudumu katika imani yao
ya kweli.
3. Uwashike mkono na kuwalinda wakatekumeni wote wanaojiandaa kwa Ubatizo, ili waingie katika Kanisa lako na
kuishi maisha mapya ya mwanga.
4. Uwapokee marehemu wetu na kuwaingiza katika nyumba yako ya milele huko mbinguni.
Ee Mwezaji wa yote, uyapokee maombi yetu haya na hata yale tusiyothubutu kuyataja. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.