JUMATATU JUMA LA 7 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa,
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.
Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.
Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:89-96 XII Sheria ya Mungu hutegemewa
Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yoh.13:34)
Neno lako, Ee Mungu, ladumu milele;*
limethibitika juu mbinguni.
Uaminifu wako wadumu vizazi vyote,*
umeiweka dunia mahali pake, nayo yadumu.
Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo,*
kwa sababu vyote ni watumishi wako.
Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu,*
ningalikwisha angamia kwa taabu zangu.
Sitasahau kamwe maagizo yako,*
maana kwa hayo umenipa uhai.
Mimi ni wako, unisalimishe,*
maana nimejitahidi kuzishika amri zako.
Waovu wanivizia wapate kuniua;*
lakini mimi nitazitafakari sheria zako.
Nimetambua kila kitu kina mpaka wake,*
lakini agizo lako halina mpaka.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.71 Mungu tumaini la wazee
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida (Rom.12:12)
I
Ee Mungu, nimekukimbilia wewe;*
usiniache kamwe niaibike.
Kwa uadilifu wako uniopoe, uniokoe;*
unitegee sikio lako, unisalimishe!
Uwe mwamba wangu wa kukimbilia,/
ngome imara ya kunisalimisha;*
kwani wewe ni mwamba na ngome yangu.
Uniokoe, Ee Mungu wangu, mikononi mwa waovu;*
uniokoe kutoka kwa wabaya na wakatili.
Maana wewe Bwana u peke yako tegemeo langu,*
Ee Mungu, nimekutumainia tangu ujana wangu;
nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu,/
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu.*
Daima nakusifu wewe.
Kwa wengi nimekuwa mfano wa kushangaza;*
lakini wewe u kimbilio langu imara.
Kinywa changu kimejaa sifa zako,*
na utukufu wako mchana kutwa.
Wakati wa uzee usinitupe;*
niishiwapo na nguvu usiniache.
Maana adui zangu wananisema;*
wanaonivizia wanashauriana,
na kusema: “Mungu amemwacha;/
mfuateni na kumkamata,*
kwani hakuna wa kumwokoa!“
Usikae mbali nami, Ee Mungu;*
uje hima kunisaidia, Ee Mungu wangu.
Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa;*
wenye kunitakia mabaya wapate aibu na dhihaka.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Lakini mimi nitasubiri kwa tumaini;*
tena nitakusifu zaidi na zaidi.
Mimi nitasimulia matendo yako ya haki,/
nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu;*
ijapokuwa yanapita akili yangu.
Nitaanza na matendo yako makuu, Ee Bwana Mungu*
nitatangaza wema wako peke yako.
Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu*
tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu.
Usiniache, Ee Mungu, hata nikiwa mzee mwenye mvi,*
mpaka nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako.
Uwezo na uadilifu wako, Ee Mungu,*
vimefika mpaka mawinguni.
Wewe umefanya mambo makuu mno.*
Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
Umeniletea taabu na shida nyingi,*
lakini utanipatia tena uzima na kuniinua.
Utaniongezea heshima yangu,*
na kunifariji tena.
Ndipo nitakusifu kwa kinanda,*
kwa sababu ya uaminifu wako, Ee Mungu wangu;
nitakuimbia sifa kwa kinubi,*
ewe Mtakatifu wa Israeli.
Nitashangilia ninapoimba sifa zako;*
nitaimba kwa moyo wote, maana umeniokoa.
Nitasimulia uadilifu wako mchana kutwa,/
maana walionitakia mabaya,*
wameona aibu na fedheha.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Ufu.1:17-18
Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini
tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninayo mamlaka juu ya kifo na kuzimu.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Kol.2:9,10a,12
Ndani yake Kristo, katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, nanyi mmepewa uzima
kamili katika kuungana naye. Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo
mlifufuliwa pia pamoja naye kwa imani yenu katika nguvu ya Mungu, ambaye alimfufua Kristo kutoka
wafu.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 2Tim.2:8,11
Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Injili
ninayoihubiri. Usemi huu ni wa kweli: “Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye.".
K. Hii ndiyo siku iliyofanywa na Bwana, aleluya.
W. Tufurahi na tushangilie, aleluya.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, utushushie neema ya Roho Mtakatifu, ili tuweze kuzingatia matakwa yako
kiaminifu, na kuyadhihirisha kwa kuishi kitakatifu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo
Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.