JUMATATU JUMA LA 7 PASAKA
MASOMO

SOMO: Mdo.19:1-8
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, kwa ubatizo wa Yohane. Paulo akasema, Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akahojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.68:1-6
1. Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika,
Nao wamchukiao huukimbia uso wake.
Kama moshi upeperushwavyo,
Ndivyo uwapeperushavyo wao;
Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto,
Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.

(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Au:
Aleluya.

2. Bali wenye haki hufurahi,
Na kuushangilia uso wa Mungu,
Naam, hupiga kelele kwa furaha.
Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake,
Shangilieni mbele zake. (K)

3. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
Mungu katika kao lake takatifu.
Mungu huwakalisha wapweke nyumbani;
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa;
Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. (K)

SHANGILIO: Mt.28:19,20
Aleluya, aleluya,
Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
mimi nipo pamoja nanyi siku zote,
hata ukamilifu wa dahari.
Aleluya.

INJILI: Yn.16:29-33
Wanafunzi walimwambia Yesu: Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. Yesu akawajibu, Je! mnasadiki sasa? Tazama. saa yaja, naam, imekwisha kuja ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.

MAOMBI
Ee Roho Mtakatifu uliyeahidiwa na Bwana wetu Yesu Kristo kabla ya kupaa kwake mbinguni kwa Baba, na uliyewajia zamani mitume kule chumbani, twakuomba:

Kiitikio: Roho Mtukufu, utusikie.
1. Wewe ni Mwalimu mkunjufu unayetufundisha utakatifu, pamoja nawe hatutakosa imani tunapokaa Kanisani. Nuru yako idumu daima ndani ya Kanisa lako.

2. Ewe Chemchemi ya mapaji yote, utushushie hekima ili tukupende daima; na utujalie akili tuifahamu imani.

3. Ndiwe mwezaji wa yote, utusaidie kwa shauri tupate kupambanua mambo na kuchagua vizuri. Utujalie na nguvu, tupate kupambana na shetani kwa uhodari.

4. Utujaze elimu na mafundisho ya imani. Utuwashie moyo wa ibada na uchaji wa Mungu.

Ee Mungu, umefundisha mioyo ya waamini kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Utujalie katika Roho huyo kutambua na kupendelea mema na kufurahia daima faraja yake. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.