JUMATATU JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.
Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.
Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.
Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.
Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.
Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.
Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.
2 (33)
Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.
E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!
Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.
Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.
Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.
Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.
Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.
3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;
Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;
Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.
Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal
4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.
Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.
Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.
Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434
5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.
Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.
Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930
ANT. I: Bwana atakuwa nuru yenu daima; Mungu wenu atakuwa utukufu
wenu, alaluya.
Zab.123 Kuomba huruma.
Vipofu wawili...walipaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuonee huruma!" (Mt.20:30)
Ninakuinulia macho yangu, Ee Mungu*
unayekaa huko juu mbinguni.
Kama watumishi wamtegemeavyo bwana wao,*
kama mjakazi amtegemeavyo bibi yake,
ndivyo tunavyokutegemea wewe, Ee Mungu, Mungu wetu,*
mpaka hapo utakapotuonea huruma.
Utuhurumie, Ee Mungu, utuhurumie,*
maana tumedharauliwa mno.
Tumedharauliwa na wadhalimu wenye kiburi,*
tumepuuzwa vya kutosha na matajiri.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Bwana atakuwa nuru yenu daima; Mungu wenu atakuwa utukufu
wenu, alaluya.
ANT. II: Mtego umevunjwa, nasi tumeokoka, aleluya.
Zab.11 Mungu kinga yetu
Bwana alimwambia Paulo katika ono: "Usiogope,... maana mimi nipo pamoja nawe" (Mate.18:9-10)
Haya Israeli, sasa useme:*
"Kama Mungu asingalikuwa upande wetu,
kweli Mungu asingalikuwa upande wetu,*
wakati ule tuliposhambuliwa na watu,
hakika tungalimezwa wazima-wazima,*
wakati hasira zao zilipotuwakia.
Hapo tungalikumbwa na gharika,/
tungalifunikwa na mto wa maji,*
mkondo wa maji ungalituchukua.“
Atukuzwe Mungu,*
asiyetuacha makuchani mwao.
Tumeponyoka kama ndege*
katika mtego wa wawindaji!
Mtego umeteguliwa,*
nasi tukaokoka.
Msaada wetu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Mtego umevunjwa, nasi tumeokoka, aleluya.
ANT. III: Nitakapoinuliwa kutoka duniani, nitawakusanya watu wote
kwangu, aleluya.
WIMBO: Ef.1:3-10 Azimio la Mungu kuhusu wokovu
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,*
Mungu alituteua tuwe wake
katika kuungana na Kristo/
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
Kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Nitakapoinuliwa kutoka duniani, nitawakusanya watu wote
kwangu, aleluya.
SOMO: Rom.8:14-17
Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, Roho mliyempokea si Roho
mwenye kuwafanya ninyi watumwa na kuwatia tena hofu; sivyo, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya
ninyi kuwa watoto wa Mungu, na kwa nguvu ya huyo Roho sisi tunaweza kumwita Mungu "Aba yaani
Baba yangu! Naye Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa
Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake,
na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki
pia utukufu wake.
KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Roho Mtakatifu, Msaidizi, atabaki kati yenu, na atakaa ndani yenu, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Roho Mtakatifu, Msaidizi, atabaki kati yenu, na atakaa ndani
yenu, aleluya.
MAOMBI
Kristo aliwajaza mitume na Kanisa lote faraja ya Roho Mtakatifu. Katika masifu haya ya jioni
tumpe shukrani zetu.
W. Bwana, ulifariji Kanisa lako, na utufanye tuwe na shukrani.
Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu, umewachagua mapadre wawe wafanyakazi wenzako;
- kwa njia ya kazi yao ya wokovu, uwafikishe watu wote kwa Baba. (W.)
Uwe katika mioyo ya matajiri, na katika maisha ya fukara;
- uwatie watu moyo wa kusaidiana katika shida zao zote. (W.)
Uyajulishe mataifa yote injili yako;
- uurejeze umoja wa wanadamu ambao ulivunjika. (W.)
Umtume Roho wako Mtakatifu, afute machozi ya ulimwengu;
- tunaomba huyo Mfariji ageuze huzuni iwe furaha. (W.)
Uwaondolee marehemu dhambi zao;
- uwapalize mbinguni, na kuwaingiza katika jumuiya ya watakatifu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, utushushie neema ya Roho Mtakatifu, ili tuweze kuzingatia matakwa yako kiaminifu,
na kuyadhihirisha kwa kuishi kitakatifu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.