JUMATATU JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana ametuahidia Roho Mtakatifu: njooni, tumwabudu, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.
Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.
Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.
Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.
Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.
Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.
Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.
2 (33)
Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.
E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!
Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.
Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.
Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.
Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.
Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.
3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;
Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;
Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.
Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal
4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.
Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.
Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.
Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434
5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.
Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.
Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930
ANT. I: Moyo wangu na roho yangu, humfurahia Mungu aliye hai, aleluya.
Zab.84 Hamu ya kuwapo nyumbani mwa Mungu
Hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja (Ebr.13:14)
Napenda mno makao yako,*
Ee Mungu mwenye nguvu!
Natamani kuwa Hekaluni mwa Mungu./
Kwa moyo na mwili wangu wote,*
namshangilia Mungu aliye hai.
Hata shomoro wamepata makao kwako;/
mbayuwayu wamejenga viota kwako,*
na kuweka makinda yao madhabahuni pako.
Ewe Mungu mwenye nguvu,*
Mfalme wangu na Mungu wangu!
Wana heri wakaao nyumbani mwako,*
ambamo waweza kukusifu daima.
Wana heri wanaopata nguvu kwako,*
wanaotamani kwenda kuhiji Mlima Sion.
Wapitapo katika bonde kavu,/
hulifanya kuwa chemchemi,*
na mvua za kwanza hulijaza madimbwi.
Wanaendelea kupata nguvu waendapo;*
watamwona Mungu wa miungu katika Sion.
Ee Mungu mwenye nguvu, sikia sala yangu.*
Unisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
Umwangalie kwa wema, Ee Mungu wetu,*
umwangalie mfalme uliyemteua.
Siku moja Hekaluni mwako,*
ni bora kuliko siku elfu mahali pengine;
hata kusimama mlangoni pa nyumba yako,*
kuliko kukaa kwa watu waovu.
Mungu ni mlinzi wetu na mfalme mtukufu;*
hutuneemesha na kutujalia fahari.
Mungu hawanyimi chochote chema,*
wale ambao wanaishi bila hatia.
Ee Mungu mwenye nguvu,*
heri wale wanaokutumainia wewe!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Moyo wangu na roho yangu, humfurahia Mungu aliye hai, aleluya.
ANT. II: Hekalu la Bwana ni kuu; watu wote watamwabudu humo, aleluya.
WIMBO: Isa.2:2-5 Mlima wa nyumba ya Bwana utainuliwa juu ya vilima
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu (Ufu.15:4)
Na itakuwa katika siku za mwisho,/
mlima wa nyumba ya BWANA*
utawekwa imara juu ya milima,
nao utainuliwa juu ya vilima;/
na mataifa yote*
watauendea makundi makundi:
Na mataifa mengi watakwenda na kusema,/
Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA,*
nyumbani kwa Mungu wa Yakobo,
naye atatufundisha njia zake,*
nasi tutakwenda katika mapito yake;
maana katika Sion itatoka sheria,*
na neno la BWANA katika Yerusalemu.
Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi,*
atawakemea watu wa kabila nyingi;
nao watafua panga zao ziwe majembe,*
na mikuki yao iwe miundu;
taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine,*
wala hawatajifunza vita tena kamwe.
Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni,*
twende katika nuru ya BWANA.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Hekalu la Bwana ni kuu; watu wote watamwabudu humo, aleluya.
ANT. III: Yatangazieni mataifa: 'Mungu ni mfalme,' aleluya
Zab.96 Mungu mfalme na hakimu
Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi, na mbele ya Mwana-Kondoo
(Ufu.14:3)
Mwimbieni Mungu, wimbo mpya!*
Mwimbieni Mungu, ulimwengu wote!
Mwimbieni Mungu na kulisifu jina lake./
Tangazeni kila siku habari njema*
kwamba ametuokoa.
Yatangazieni mataifa utukufu wake,*
na matendo yake makuu kwa watu wote.
Maana Mungu ni mkuu, anasifika sana;*
astahili kuheshimiwa zaidi kuliko miungu yote.
Miungu ya mataifa mengine si kitu;*
lakini Mungu aliziumba mbingu.
Utukufu na fahari vyamzunguka;*
enzi na uzuri vyalijaza Hekalu lake.
Mpeni Mungu heshima, enyi jamii zote za watu;*
sifuni utukufu na enzi yake.
Lisifuni jina tukufu la Mungu;*
leteni sadaka na kuingia Hekaluni mwake.
Mwabuduni Mungu anapotokea,*
tetemeka mbele yake, ee dunia nzima.
Yaambieni mataifa: “Mwenyezi ni mfalme!/
Ameufanya ulimwengu imara, hautatikisika.*
Atawahukumu watu kwa haki."
Furahini, enyi mbingu na dunia!*
Bahari na zivume pamoja na vyote vilivyomo!
Furahini, enyi mashamba na vyote vilivyomo!*
Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha,
Mungu atakapotokea kutawala dunia.*
Naam, atawatawala watu kwa haki na usawa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Yatangazieni mataifa: 'Mungu ni mfalme,' aleluya
SOMO: Rom.10:8b-10
Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako, nao ndio ile imani
tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana, na kuamini moyoni mwako
kwamba Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Maana twaamini kwa moyo na kufanywa kuwa wenye
uhusiano mwema na Mungu; na twakiri kwa midomo yetu na kuokolewa.
KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Ulimwenguni mtapata masumbuko. Lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Ulimwenguni mtapata masumbuko. Lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda
ulimwengu, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, aliyeahidi kwamba Baba angemtuma Mfariji kwa jina lake.
W. Utupatie Roho wako Mtakatifu.
Tunakushukuru wewe, Kristo Bwana wetu, na kwa njia yako tunatoa shukrani kwa Baba katika Roho Mtakatifu;
- kila kitu tutakachofanya leo na kitangaze jina lako. (W.)
Roho wako Mtakatifu na akae ndani yetu;
- atufanye tuwe viungo hai vya mwili wako. (W.)
Usituruhusu kuwahukumu au kuwadharau ndugu zetu;
- utufanye tukumbuke kwamba siku moja sote tutasimama mbele ya kiti chako cha hukumu. (W.)
Katika kuamini kwetu, utujaze furaha na amani yote;
- kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, uongeze upeo wa matumaini yetu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, utushushie neema ya Roho Mtakatifu, ili tuweze kuzingatia matakwa yako kiaminifu,
na kuyadhihirisha kwa kuishi kitakatifu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.