JUMATATU JUMA LA 5 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.14:5-18
Siku zile, palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao,
kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, mji wa
Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra palikuwa
na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo
alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa,
akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona
aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya
wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu
ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka
kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua
nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona
mnafanya haya? Sisi nasi ni wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na
kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari
na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao
wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni,
na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia
makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.115:1-4,15-16(K)1
1. Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi,
Bali ulitukuze jina lako.
Kwa ajili ya fadhili zako,
Kwa ajili ya uaminifu wako.
Kwa nini mataifa kusema,
Yuko wapi Mungu wao?
(K) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi,
Bali ulitukuze jina lako.
2. Lakini Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu. (K)
3. Na mbarikiwe ninyi na Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
Mbingu ni mbingu za Bwana,
Bali nchi amewapa wanadamu. (K)
SHANGILIO: Kol.3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo,
yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko,
ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI: Yn.14:21-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye;
naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote),
akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu
akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja
kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia
silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.
Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote,
na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
MAOMBI
Ndugu, kumpenda Mungu maana yake ni kutimiza mapenzi yake. Hii ni pamoja na kumtendea jirani yale ambayo
sisi wenyewe tunapenda kutendewa. Hiyo siyo kazi rahisi. Kwa vile tunahitaji huruma ya Mungu, tuombe:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Maajabu yanayofanywa na viongozi wako wa Kanisa daima yatukumbushe nafasi ya Roho Mtakatifu katika
nafsi ya kila mbatizwa.
2. Injili yako ienee kwa mataifa yote, ili watu waache mambo ya ubatili na kukugeukia wewe Mungu uliye hai.
3. Utuimarishe sisi sote tuliopokea Roho Mtakatifu katika sakramenti mbalimbali, ili tuueneze upendo
wako mahali pote na wakati wowote.
4. Uwape marehemu wetu raha ya milele huko mbinguni.
Ee Mungu uliyetutendea mema tangu zamani zilizopita, utujalie hayo na utusaidie kukushuhudia kwa matendo
yakupendezayo wewe na jirani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.