JUMATATU JUMA 5 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Dan.13:1-9,15-17,19-30,33-62
Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti
Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha
binti yao sawa sawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba
yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa ni mwenye heshima kupita
wengineo wote.
Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa
namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa
kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote
wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko.
Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa
sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku
anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao,
wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa
walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na
wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa na mtu yeyote
isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake,
Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge.
Mara wale wajakazi
walipokwisha kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango
ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali
na ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndiyo
sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema, Nimesongwa pande zote, maana
nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali
niangukie katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu.
Mara Susana
akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao
akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele
bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini
wale wazee waliisimulia hadithi yao nao watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana
hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote.
Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa
Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha.
Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda
kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye
huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe
uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama
wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya
kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu.
Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na
wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea
kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa
bustani, tuliona ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza
kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka. Bali huyu
tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu.
Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana
akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote
yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini
sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi. Naye Bwana akaisikia
sauti yake.
Kwa hiyo alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja,
jina lake Daniel; nae akapaza sauti yake akasema, 'Mimi simo, mimi sina hatia kwa habari ya
damu yake mwanamke huyu'. Mara wote wakamgeukia, wakasema, "Maneno hayo usemayo maana yake nini?"
Akasimama katikati, akasema, "Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumuhukumu binti Israeli
bila kuhoji wala kupata Hakika ya kweli? rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo". Basi
watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, "njoo uketi kati yetu, utujulishe
habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima ya mzee". Hapo Danieli akawaambia, wawili hawa
watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa akamwita mmoja wao, akamwambia, "Ewe uliyepata
kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki,
kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, asiye na hatia mwenye haki
usimwue. Haya! basi wewe ulimuona kwa macho, useme, chini ya mti gani uliwaona wakikaa
pamoja?" Naye akajibu, "Chini ya msandarusi." Danieli akasema, "Hakika umesema uongo juu ya
kichwa chako mwenyewe; maana sasa hivi malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga,
akukate vipande viwili." Akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta huyo mwingine, akamwambia,
"Ewe mzao wa Kaanani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako.
Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda
hakuweza kustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe usema; chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja?"
Naye akajibu "Chini ya mkwaju." Danieli akamwambia, "Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya
kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate
vipande viwili; ili awaangamize wote wawili." Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa
nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio.
Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata
vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa
ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua, na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.25:4-9,(K)10
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
2. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SHANGILILO:
Maneno yako, Ee Bwana,
ni roho, tena ni uzima,
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
INJILI: Yn.8:1-11
Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi
kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha.
Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.
Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa
alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo
wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake
katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni
mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.
Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata
wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua
asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je!
Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi
sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.
MAOMBI
Yesu ni nuru ya ulimwengu, lakini wale aliokuja kuwaangazia hawakutaka kumpokea ingawa ushuhuda wake ulikuwa wa
kweli. Tumwombe Mungu ili tupate kutimiza matakwa yake. Ee Mungu twakuomba:
Kiitikio: Kwa huruma yako Bwana, utusikie.
1. Baba Mtakatifu, maaskofu na mapadre wazidi kuushuhudia ukweli wa neno lako na wa Kanisa lako.
2. Vyombo vya sheria vidumishe haki, amani na uhuru wa watu kujieleza na kuyapima mambo sawasawa kabla ya kutoa
hukumu kwa raia.
3. Utupe moyo wa kudumu katika sala; hasa pale tunaposongwa na majaribu makali.
4. Wote ambao, bila kosa lolote, wananyimwa haki yao ya kuishi, wajikabidhi kwa Kristo aliyesema: “Baba, mikononi
mwako naiweka roho yangu.”
Ee Bwana, nuru yako iangaze mioyoni mwetu, ili tuutambue ukweli na kuushuhudia mbele ya watu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.