JUMATATU JUMA LA 4 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.11:1-18
Siku zile mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa
nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara
wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza
kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono;
chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.
Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni,
nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.
Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa
kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene
wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na
tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka
Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja
nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama
nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia
maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu
akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema,
Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi
Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani
niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi,
Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.42:1-2;43:2-3(K)42:2
1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.
Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai,
Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu,
Mungu aliye hai.
2. Kwa kuwa Wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu;
kwa nini umenitupa?
Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea? (K)
3. Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako. (K)
SHANGILIO: Ufu.1:5
Aleluya, aleluya,
Ee Kristo,
yu shahidi aliye mwaminifu
mzaliwa wa kwanza wa waliokufa,
na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.
INJILI: Yn.10:1-10
Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo,
lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji
wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake
kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale
kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa
maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo
hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa
kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi
mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji
ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
MAOMBI
Ndugu, sisi tumefundishwa na tunaamini kuwa kutahiriwa au kutotahiriwa kwa mwili siyo kitu, bali
tuwe viumbe vipya. Lakini twahitaji msaada wa Mungu tupate kupambana na malimwengu yanayotusonga
dhidi ya imani yetu ya kikristo. Tuombe:
Kiitikio: Kwa huruma yako, pokea ombi letu.
1. Viongozi wa dini mbalimbali wakwepe malumbano yoyote yasiyoendana na maisha mapya ya ufufuko.
2. Watawala wa dunia wawapokee wainjilishaji kwa furaha na moyo wa shukrani.
3. Wote wanaoitwa kulitangaza Neno lako waitike; na wachungaji wote wawaongoze kondoo wako kwenye
malisho mema mpaka kwenye mlango wa mbingu.
4. Uwaponye wagonjwa na uwafufue wafu wetu wakashiriki ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi, mateso na kifo.
Ee Mungu, wewe wanena nasi kwa njia mbalimbali. Utufanye wasikivu zaidi na zaidi kwa viongozi wetu
wanaokujua wewe na kumwakilisha Mwanao aliye Mlango, Njia, Ukweli na Uzima. Milele na milele. Amina.