JUMATATU JUMA LA 3 PASAKA
MASOMO

SOMO: Mdo.2:14,22-32
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi; wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahli hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.

WIMBO WA KATIKATI: ZAB.119:23-24,26-27,29-30(K)1
1. Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
Shuhuda zako ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.

(K) Heri walio kamili njia zao.

2. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundisha amri zako.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako. (K)

3. Uniondolee njia ya uongo,
Unineemesha kwa sheria yako.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)

SHANGILIO: Lk.24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristu kupata mateso haya,
na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.

INJILI: Yn.6:22-29
Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja; tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru. Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.

MAOMBI
Ndugu, mkutano wa watu ulimfuata Yesu hata ukamkuta ng'ambo ya bahari kwa sababu kabla yake aliwapa mikate wakashiba. Hata sisi tunahitaji msaada wa Mungu tupate kuwa mashahidi waaminifu wa Injili yake. Basi, tuombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwape viongozi wetu wa Kanisa neema na uwezo wa kuwa mfano bora katika kufanya maajabu na ishara kubwa katika watu wanaowaongoza.

2. Uzuie ushindani usio na manufaa yoyote kimwili au kiroho kati ya mataifa, ili watu waufuate ukweli wako.

3. Sisi sote tuzitende kazi zako, Ee Mungu, kwa kumwamini mwanao uliyemtuma kwetu.

4. Uwahesabie haki marehemu wetu wapate kung'ara mbele yako kama uso wa malaika.

Ee Baba yetu mwema, utudumishe katika kuepa kufuru za mambo matakatifu, tukashike amri zako na desturi zile tu ambazo zinakubalika mbele yako. Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.