JUMATATU JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Mak.1:10-15,41-43,54-57,62-64
Kulichipuka chipukizi chenye dhambi, ndiye Antioko Epifani, mwana wa mfalme Antioko, ambaye alikuwa
amewekwa amana kwa Warumi. Naye alitawalishwa katika mwaka wa mia thelathini na saba wa enzi ya
Wayunani. Siku zile walitokea wahalifu sheria katika Israeli, wakashawishi wengi, wakisema, Twende
tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka, maana tangu tulipofarakana nao misiba mingi imetupata.
Jambo hilo likapendeza machoni pao, hata watu Fulani wakafanya hima kwenda kwa mfalme, naye akawapa
ruhusa kuzifuata kawaida za mataifa. Wakafanya kiwanja cha michezo Yerusalemu kama kawaida ya mataifa,
wakajifanya kana kwamba hawakutahiriwa wakajitenga na agano takatifu. Hivyo walijiunga na mataifa
na kujiuza wafanye uovu. Mfalme Antioko akaziandikia milki zake zote, kwamba wote wawe taifa moja,
kila mtu aache sheria zake za asili. Watu wote wa mataifa wakaikubali amri ya mfalme, hata wengi
katika Israeli walifuata ibada yake, wakitoa dhabihu kwa miungu ya uongo na kutia unajisi Sabato.
Siku ya ishirini na tano ya Kislevu, mwaka wa mia arobaini na tano, waliweka chukizo la uharibifu
juu ya madhabahu, na katika miji ya Uyahudi kila upande walijenga vimadhabahu vya miungu, wakavukiza
uvumba milangoni pa nyumba na njiani. Na vitabu vya sheria walivyovipata waliviparua vipande vipande
wakaviteketeza. Mtu yeyote aliyepatikana na kitabu, au aliyeonekana anaifuata sheria, alihukumiwa
kufa kama alivyoamuru mfalme. Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile
vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kutiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano
takatifu. Wakafa. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:53,61,134,150,155,158 (K)88
1. Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
Kamba za wasio haki zimenifunga,
Sikuisahau sheria yako.
(K) Unihuishe kwa fadhili zako,
nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
2. Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu,
Nipate kuyashika mausia yako.
Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
Wamekwenda mbali na sheria yako. (K)
3. Wokovu u mbali na wasio haki,
Kwa maana hawajifunzi amri zako.
Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
Kwa sababu hawakulitii neno lako. (K)
SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!
INJILI: Lk.18:35-43
Yesu alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka;
na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.
Akapiga kelele, akisema, Yesu Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea
ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu
akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema,
Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; Imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona,
akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu Baba, umetuletea neno lenye kutuandaa kwa siku ya mwisho. Hivyo, huku
tukikushukuru, tunakuomba tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee shukrani zetu kwa kuwa Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi
wengi wa Kanisa wanafanya jitihada za kuieneza imani aliyotuachia Mwanao. Ee Bwana.
2. Uwakinge waamini wako na chachu ya kipagani, ili walishike agano lako takatifu, na
kukutumainia Wewe katika maisha yote. Ee Bwana.
3. Utujalie imani thabiti kama ya yule kipofu wa Yeriko, tupate kuponywa udhaifu wetu
na kuona njia iendayo kwako. Ee Bwana.
4. Kwa namna ya pekee umsaidie kila aliyeuacha upendo wake wa kwanza, umkumbushe ni wapi
alikoanguka; apate kutubu na akayafanye matendo ya kwanza. Ee Bwana.
5. Imani waliyokuwa nayo ndugu zetu marehemu iwaponye na dhambi wapate kuingia
kwako mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewapokea na kuwaponya wote wanaokujia kwa moyo mnyofu na imani
thabiti, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.