JUMATATU JUMA 32 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Hek.1:1-7
Pendeni haki, enyi waamuzi wa dunia; Tafakarini habari za Bwana kwa moyo mwema. Na kumtafuta katika
unyofu wa moyo. Kwa sababu huonekana nao wasiomjaribu, na kufunuliwa kwao wasiokosa kumwamini. Mradi
fikira zilizopotoka hutenga wanadamu na Mungu, na enzi yake ikijaribiwa, huwafadhaisha wajinga. Hekima
haiingii katika roho ya mtu awazaye maovu, wala haikai katika mwili wa mtu aliyefungwa rehani na
dhambi. Kwa kuwa roho takatifu yenye maadili huikimbia hila, hubumburuka kujiepusha na fikira zisizo
na akili, hufadhaika kuingiwa na udhalimu. >Maana Hekima ni roho ambayo huwapenda wanadamu, wala
haimwachilii mkufuru hatia ya midomo yake; kwa sababu Mungu huvishuhudia viuno vyake, na kuusimamia
hasa moyo wake, na kuusikiliza ulimi wake. Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviungamanisha
viumbe vyote hujua maana ya kila sauti.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-10
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze katika njia ya milele, Ee Bwana.
2. Maana hamna neno ulimini mwangu
Usilolijua kabisa, Bwana.
Umenizingira nyuma na mbele,
Ukaniwekea mkono wako.
Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi,
Hayadirikiki, siwezi kuyafikia. (K)
3. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko,
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. (K)
4. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)
SHANGILIO: 2Kor.5:19
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristu,
akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:1-6
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja
kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusaga lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini,
kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni. Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu
msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu,
msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na Imani kiasi
cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka ukapandwe baharini, nao ungewatii.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, uliyetujalia zawadi ya ufunuo mpana zaidi
kuliko ule wa mitume, twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ili Baba Mtakatifu F.,
Askofu wetu F. na wakleri
wote wazidi kuwaonya watu wako dhidi ya
usababishaji makwazo; na kuhimiza upendo,
hekima na haki. Ee Bwana.
2. Ili taifa lako lipate daima viongozi wenye sifa
njema; wakaribishaji na wema, wenye kiasi na haki,
watakatifu, wenye imani sahihi, na wenye uwezo
wa kufundisha watu na kukemea maovu. Ee Bwana.
3. Ili waamuzi wa dunia wapende haki, watafakari habari
zako Bwana kwa moyo mwema, na kukutafuta katika
unyofu wa moyo. Ee Bwana.
4. Ili tujaliwe hekima yako ya kimungu, tupate kuwaza,
kusema na kutenda yakupendezayo Wewe na jirani zetu. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wafutiwe dhambi zao na kupewa
heri ya milele katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayejifunua kwao wakuaminio, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.