JUMATATU JUMA 30 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rum.8:12-17
Kama ni hivyo, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili; kwa maana kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate kutukuzwa pamoja naye.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.68:1,3,5-6,19-20 (K)20
1. Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha.

(K) Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa.

2. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika ko lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa. (K)

3. Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu. Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini. (K)

SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu,
li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!

INJILI: Lk.13:10-17
Siku ya sabato Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akamjibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, Je! Hamfungi ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ndio wana wa Mungu, tumwombe Mungu mwenyewe tukisema:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie Wakleri wote kuwaandaa vema wapokeaji Ubatizo na Sakramenti zingine, wapate kukujua vya kutosha na kuyapokea maongozi na mapaji yako. Ee Bwana.

2. Viongozi wetu wahakikishe vyombo vya dola vinasimamia sheria iletayo uhuru wa kweli dhidi ya wahalifu, wanaofanya mambo machafu na kuwadhihaki wenye mamlaka. Ee Bwana.

3. Uwakomboe wakosefu kutoka katika utumwa wa dhambi na shetani, na kuwaingiza katika utawala wa wana wako. Ee Bwana.

4. Utuepushe na unafiki na kutujalia roho ya utii wa sheria yako iletayo wokovu. Ee Bwana.

5. Marehemu waliokombolewa na Mwanao, wasamehewe dhambi zao, wapate kulia Aba kwa furaha huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu Baba unayetaka tuvumilie yote kwa ajili yako, utujalie hayo yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.