JUMATATU JUMA LA 2 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.4:23-31
Walipofunguliwa, Petro na Yohane wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa
na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema,
Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena
kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na
makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya
Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa
Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili
wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana,
yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono
wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha
kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno
la Mungu kwa ujasiri.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.2:1-3,4-7A,7B-9 (K)13
1. Mbona mataifa wanafanya ghasia,
Na makabila wanatafakari ubatili?
Wafalme wa dunia wanajipanga,
Na wakuu wanafanya shauri pamoja,
Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.
Na tuvipasue vifungo vyao,
Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.
(K) Heri wale wanaomkimbilia Mungu.
Au:
Aleluya.
2. Yeye aketiye mbinguni anacheka,
Bwana anawafanyia dhihaka.
Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake,
Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.
Nami nimemweka mfalme wangu
Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. (K)
3. Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)
SHANGILIO: Lk.24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya
na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.
INJILI: Yn.3:1-8
Palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia,
Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi
uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu
asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa,
akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia,
Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili;
na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.
Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na
hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.
MAOMBI
Ee Mungu uliyezifanya mbingu na nchi na vitu vyote vilivyomo, na uliyenena kwa Roho Mtakatifu kwa
vinywa vya baba zetu, twajua kuwa Mwanao Yesu Kristo ndiye Mwalimu wetu pekee aliyetufundisha namna
ya kuhusiana nawe. Kwa ushindi na ujasiri aliotudhihirishia, twaja kwako tukisema:
1. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyefanya kazi miongoni mwa mitume, uwajalie viongozi wote wa Kanisa
kuhubiri neno lako kwa ujasiri katika ulimwengu huu wenye ghasia za kila aina.
2. Uwape wote wenye mamlaka ya kisiasa au kiserikali ari ya kuitambua na kuijali nafasi ya wahubiri wa
neno lako, katika kuyastawisha maisha ya watu wako kimwili na kiroho.
3. Wale wote waliotiwa mafuta kwa Ubatizo wasichoke kuyafuata mashauri yako uliyoyakusudia tangu zamani
za baba zetu, na ukatudhihirishia utabiri wake kwa maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Mwanao.
4. Uwajalie ndugu zetu marehemu waliozaliwa kwa maji na kwa Roho kuuingia ufalme wako huko mbinguni.
Ee Baba Mwema, utusaidie kuepa dhambi kwani, kwa Ubatizo na kwa fumbo la Paska, tumefanywa wapya katika
Roho Mtakatifu; na utusaidie kuyatimiza yale tu yakupendezayo wewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.