JUMATATU JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.4:20-25
Ibrahimu akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza
Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake
kuwa ni haki. Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili
yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu;
ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.
WIMBO WA KATIKATI: Lk.1:69-75 (K)68
1. Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli.
2. Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu; (K)
3. Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (K)
SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao
hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya!
INJILI: Lk.12;13-21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.
Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia,
Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.
Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza
moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya
hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote
na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa
miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu
wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye
nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.
--------------
--------------
MAOMBI
Kwa vile pendo la Mungu limekwisha kumiminwa
mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu, tumehesabiwa haki
pasipo mastahili. Tumsifu na kumtukuza Mungu
tukisema:-
Kiitikio: Utukuzwe, Ee Mungu.
1. Kwa kuwa umelijalia Kanisa lako Maaskofu na
apadre ambao wamehesabiwa haki ya kuushiriki ukuhani
wa Mwanao Yesu Kristo.
2. Kwa kuwa hata viongozi wa serikali ni kazi yako,
wameumbwa ili watende matendo mema, ambayo tokea mwanzo
uliyatengeneza ili tuende nayo.
3. Kwa kuwa watu wote duniani wamehesabiwa haki ya
kuwa wazao wa Ibrahimu aliye baba yetu wa Imani.
4. Kwa kuwa sisi tunaokuamini tulipata kuhesabiwa haki
kwa Fumbo Kuu la Pasaka, lilitotimizwa na Mwanao Mpenzi Yesu Kristo.
5. Kwa kuwa hata ndugu zetu marehemu wamehesabiwa haki,
wanaombewa na sisi tulio bado hai hapa duniani, ili wapewe uzima
wa milele huko mbinguni.
Ee Mungu unayetaka tujitajirishe kwako, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.