JUMATATU JUMA 28 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.1:1-7
Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo
Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; yaani, habari za
Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana
wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika
yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa Imani, kwa ajili ya jina lake;
ambao kaitka hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu,
walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na Amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana
Yesu Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4 (K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya!
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako.
Nitaitii kwa moyo wangu wote,
Aleluya!
INJILI: Lk.11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta
ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa
Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya
hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka
nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi
watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao
walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu Kristo ambaye ni wa ukoo wa Daudi na Mkuu
kuliko Sulemani, alijidhihirisha kuwa ni Mwana wa
Mungu kwa roho ya utakatifu na kwa ufufuko wake
kutoka wafu. Tumwombe Mungu tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wote wa Kanisa wasichoke kuihubiri Injili,
ili wengi zaidi wapate kuamini na kubatizwa kwa jina la Mwanao
Yesu Kristo. Ee Bwana.
2. Uwaonye watu wasiomkiri Mwanao Yesu Kristo, wapate
kuishuhudia hekima yake na ishara zitokazo kwako. Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu kutunza neema ya utakatifu
tuliyopewa siku ya Ubatizo, tupate kustahili wokovu uliokamilishwa
kwa fumbo la Pasaka. Ee Bwana.
4. Wakristo wenzetu wanaokosa uungwana na kuyumbayumba
katika imani, wamrudie Kristo aliyewaandika huru; wasimame imara,
wala wasinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Ee Bwana.
5. Marehemu wanaongojea huruma yako wapokelewe huko
mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.