JUMATATU JUMA 27 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Yon.1:1-17;2:10
Neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige
kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi,
apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi,
akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana. Lakini Bwana
alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.
Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa
merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu;
akajilaza, akapata usingizi. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka,
ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee. Wakasemezana kila mtu na mwenzake,
Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo
kura ikamwangukia Yona. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa
sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila
gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi
kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu
wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha. Basi
wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye
akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili
yangu tufani hii imewapata. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani,
wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana. Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee
Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo
na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini,
nayo bahari ikaacha kuchafuka. Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka
nadhiri. Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki
yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.Ndipo Yona akamwomba Bwana, Mungu wake, katika tumbo la yule
samaki, Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu, Naye akaniitikia; Katika tumbo la kuzimu
naliomba, Nawe ukasikia sauti yangu. Maana ulinitupa vilindini, Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji
ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. Nami nikasema,
Nimetupwa mbali na macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. Maji yalinizunguka,
hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu; Nalishuka hata pande za
chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu
kutoka shimoni, Ee Bwana, Mungu wangu, Roho yangu ilipozimia ndani yangu, Nalimkumbuka Bwana; Maombi
yangu yakakuwasilia, Katika hekalu lako takatifu. Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo Hujitenga
na rehema zao wenyewe; Lakini mimi nitakutolea sadaka kwa sauti ya shukrani; Nitaziondoa nadhiri zangu.
Wokovu hutoka kwa Bwana. Bwana akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.
WIMBO WA KATIKATI: Yon.2:1-3,7 (K)6
1. Ndipo Yona akamwomba Bwana,
Mungu wake, katika tumbo la yule samaki,
(K) Umenipandisha nafsi yangu kutoka
shimoni Ee Bwana.
2. Akasema, Nalimlilia Bwana kwa sababu ya shida yangu,
Naye akaniitikia;
Katika tumbo la kuzimu naliomba,
Nawe ukasikia sauti yangu. (K)
3. Maana ulinitupa vilindini,
Ndani ya moyo wa bahari;
Gharika ya maji ikanizunguka pande zote;
Mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. (K)
4. Roho yangu ilipozimia ndani yangu,
Nalimkumbuka Bwana;
Maombi yangu yakakuwasilia,
Katika hekalu lako takatifu. (K)
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli,
Ee Bwana ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:25-37
Mwanasheria mmoja alisimama akamjaribu Yesu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima
wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana
Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zote;
na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka
kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka
toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha,
wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona
alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja
katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na lipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake,
akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.
Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote
utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi
aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma.
Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tuoneshe matumaini yetu kwa Mungu aliyepo,
aliyekuwako na atakayekuja, kwa kumpelekea maombi
yetu:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Baba Mtakatifu wetu F. na
wachungaji wote wa Kanisa lako wazidi kuwafundisha watu mambo ya
msingi unayotuamuru kwa ajili ya kuurithi uzima wa milele. Ee Bwana.
2. Ili watu wa mataifa yote wakishaijua nguvu yako ya
kuangamiza na kuokoa ulimwengu, wapate kuamini na kulitukuza
jina lako. Ee Bwana.
3. Ili wote wanaoitwa kuihubiri Injili, wakiisha
uitikia wito wako, waliishi neno hilo kwa mfano wa Msamaria
mwema. Ee Bwana.
4. Roho wako Mtakatifu awasaidie Wakristo kuwabaini na
kuwapuuza wahubiri wa uwongo, wanaofundisha mapokeo ya wanadamu,
kinyume na Injili ya Mwanao. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu, wakiisha safishwa dhambi zao, kwa
huruma yako kuu, wapokelewe kwako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuagiza kuwa na huruma, uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.