JUMATATU JUMA 25 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ezr.1:1-6
Ilikuwa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalame wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema
kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwambia roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata
akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi:
Bwana Mungu wa mbinguni amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika
Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Mungu wake na awe pamoja
naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli,
(yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali popote akaapo hali
ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi
ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo
wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu
wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya Bwana, iliyoko Yerusalemu.
Na watu wote, waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha,
kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari
ya mtu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.126 (K)3
1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.
Ndipo waliposema katika mataifa,
“Bwana amewatendea mambo makuu”.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
2. Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini. (K)
3. Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha.
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda,
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe,
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:16-18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo,
au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa
maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana
na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye
na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu ambaye furaha yako imekuwa daima pamoja na wanadamu,
tunakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa kuyaona matunda ya kazi
zao za kitume, wapate kutiwa moyo na ari ya kuliongoza kundi
lako katika njia ya imani. Ee Bwana.
2. Uamshe ndani ya watawala wa dunia tabia ya kuthamini
uwepo wako wa kimungu, na kuwapa watu wako uhuru wa kukuabudu
Wewe. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kuwa wakarimu kwa wenye shida ili,
kwa huduma zetu na upendo wetu kwao, wapate kukutana nawe uliye
mpaji wa vyote. Ee Bwana.
4. Tunajiombea wenyewe dhidi ya watu jeuri, wakaidi
na waovu; ili waache machukizo na njia zao mbaya; sisi tupate
amani na usalama. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu waione nuru yako isiyofifia
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu ambaye kwako hakuna lililositirika ambalo halitafunuliwa,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.