JUMATATU JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Thes.4:13-17
Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na
matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala
katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi
tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha
kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya
malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi
tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo
tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1,3-5,11-13 (K)13
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi zote.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.
2. Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana.
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu,
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. (K)
3. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
4. Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.4:16-30
Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama
ilivyokuwa desturi yake, akasimama ilia some. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo,
akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na
vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.
Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi
wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia
wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake. Wakasema, Huyu siye mwana wa
Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo
yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende hapa pia katika nchi yako mwenyewe.
akasema, Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubalika nchi yake mwenyewe. Lakini,
kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati
mbingu zilipofungwa miaka mitano na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya
hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa
na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila
Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo.
Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa
juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, wajibu wa kuihubiri Injili tuliopewa siku ya
Ubatizo unakabiliwa na changamoto nyingi. Bila msaada
wa Mungu mwenyewe hatutaweza kuutimiza sawa sawa
wajibu huo mkubwa. Tuombe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na
wachungaji wote wa Kanisa lako kuitangaza Injili yako na kuitetea
imani sahihi hasa wanapokabiliwa na upinzani mkali. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wajaliwe kusimamia vema sheria
zinazowapa watu uhuru wa kuabudu na kulitangaza jina lako. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kulishuhudia fumbo la Pasaka bila
woga katika maisha yetu ya kila siku, ili tupate tuzo siku ya
ufufuko wetu. Ee Bwana.
4. Roho wako Mtakatifu awasaidie wanaohangaika kutafuta
ukweli kwa wahubiri mbalimbali, ili imani yao isiwe katika hekima
ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu waliolala mauti wafike kwako, wapate
kuishi Nawe milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tufarijiwe na neno lako, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.