JUMATATU JUMA 21 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1The.1:2-5,8-10
Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi
kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika
Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua
uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika
Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa
ajili yenu. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila
mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lo lote. Kwa kuwa wao
wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia
Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka
mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.149:1-6 (K)4
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Bwana awaridhia watu wake.
2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Aleluya. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Mt.23:13-22
Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake: Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa
kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi
waingie. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi
kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa
jehanumu mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu
atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.
Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au ile hekalu liitakasalo
dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo
juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu
iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo
juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye
kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Bwana Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi
wa hasira, mwingi wa rehema na kweli. Tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwape viongozi wetu wa Kanisa karama ya kuwafariji
waamini wao wapatwapo na mashaka au misukosuko katika imani
yao kwako. Ee Bwana.
2. Watu wa mataifa yote wakuongokee na kukutumikia
Wewe Mungu uliye hai na wa kweli, wakiacha sanamu na yote
yanayopingana na jina lako. Ee Bwana.
3. Wabatizwa wote tujaliwe neema ya kulihubiri na
kuliishi neno lako, lipate kuvuma kote na kuwaokoa wengi. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wote wanaoteseka kwa ajili ya jina
lako, ili wahesabiwe haki na kila tunda la imani yao wapate
kuingia katika ufalme wako wa mbinguni. Ee Bwana.
5. Uwarehemu marehemu wetu na kuwaingiza katika
ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana
Ee Mungu unayetukuzwa kwa sala na matendo yetu uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.