JUMATATU JUMA 20 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Amu.2:11-19
Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.
Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine,
baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha
Bwana, akaghadhibika. Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya Bwana ikawaka juu
ya Israeli, naye ikawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono
ya adui ao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda, mkono wa Bwana
ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika
sana. Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini
nawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine wakajiinamisha
mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana;
bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na
mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa
ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa
mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao. kwa kuifuata miungu mingine ili
kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.106:34-37,39-40,43-44 (K)4
1. Hawakuwaharibu watu wa nchi
Kama Bwana alivyowaambia;
Bali walijkhanganya na mataifa,
Wakajifunza matendo yao.
(K) Ee Bwana, unikumbuke mimi,
kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
2. Wakazitumikia sanamu zao,
Nazo zikawa mtego kwao.
Naam. walitoa wana wao na binti zao
Kuwa dhabihu kwa mashetani. (K)
3. Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao,
Wakafanya uasherati kwa matendo yao.
Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake,
Akauchukia urithi wake. (K)
4. Mara nyingi aliwaponya,
Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao,
Wakadhilika katika uovu wao.
Lakini aliyaangalia mateso yao,
Aliposikia kilio chao. (K)
SHANGILIO: 1Thes.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu,
siyo kama neno la wanadamu,
bali kama neno la Mungu.
Aleluya!
INJILI: Mt.19:16-22
Mtu mmoja alimwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?
Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika
uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie
uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Yule kijana
akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa
mkamilifu, enenda ukauze ulivyonavyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha
njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa
na mali nyingi.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tunahitaji neema ya Mungu ili kuishika Amri
Kuu ya Mapendo. Basi, tumwombe tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wazidi kubuni mbinu za kuifafanua
Amri Kuu ya Mapendo, ili tukupende Wewe na jirani kwa maana
halisi na inayokubalika nawe. Ee Bwana.
2. Serikali yetu idumu katika kusimamia sheria zenye
kuleta haki na uhuru wa kweli, ili raia wote waishi kwa upendo,
amani na ustaarabu. Ee Bwana.
3. Uwaepushe watu wako na mambo yanayokiuka amri ya mapendo;
ikiwa ni pamoja na kutowahusudu watu au mali badala yako Wewe. Ee Bwana.
4. Utujalie kuzitumia mali zetu kwa upendo, ili tupate
tuzo la kuingia mbinguni. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu kuurithi ufalme wako wa milele
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuonesha mapendo ya kweli, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.