JUMATATU JUMA 19 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kum.10:12-22
Sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika
njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako
yote; kuzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri? Tazama, mbingu ni
mali za Bwana, Mungu wako, na mbingu za mbingu, na nchi, na vitu vyote vili- vyomo. Tena, Bwana
aliwafurahia baba zako, na kuwapenda, akawachagua wazao wao baada yao, naam, na ninyi zaidi ya
mataifa yote kama hivi leo. Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu. Kwa
maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye
kuogofya, asiye- pendelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. Huwafanyia yatima na mjane hukumu
ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. Basi, mpendeni mgeni, kwa sababu ninyi
wenyewe mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana
naye, na kuapa kwa jina lake. Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea
mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako. Baba zako walishukia Misri na watu
sabini; na sasa Bwana, Mungu wako, amekufanya kama nyota za mbinguni kwa wingi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.147:12-15,19-20 (K)12
1. Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
msifu Mungu wako, ec Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
amewabariki wanao ndani yako.
(K) Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
au:
Aleluya
2. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
neno lake lapiga mbio sana. (K)
3. Humhubiri Yakobo neno lake,
na Israeli amri zake na hukumu zake
Hakulitenda taifa lo lote mambo kama hayo,
wala hukumu zake hawakuzijua.
Aleluya. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema, mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima.
Aleluya!
INJILI: Mt.17:22–27
Mitume walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika
mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana. Hata walipofika
Kapernaumu, wale watozao nusushekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi
nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema,
Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa
wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru.
Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoano, ukatwae samaki yule azukaye kwanza;
na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu ametufanyizia huruma yake na kututendea
mema mengi. Na hivi tumpelekee maombi yetu. Ee Mungu
twakuomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wajaliwe kuiga mfano wa
Mwanao, wa kufundisha na kutenda yaliyo haki. Ee Bwana.
2. Watu wote na wa nyakati zote wakukiri Wewe kuwa
ndiwe Mungu wa miungu, Bwana wa mabwana, Mungu Mkuu, mwenye
kuogofya, usiyependelea nyuso za watu, wala hukubali
rushwa. Ee Bwana.
3. Waamini wote wadumishe uaminifu katika kutimiza
wajibu wao kwa Kanisa na kwa jamii, kwa kutoa michango mbalimbali,
kwa ustawi wa taifa lako kiroho na kimwili. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote upendo na ukarimu kwa wajane,
yatima, wageni na wote wenye shida. Ee Bwana.
5. Uwashirikishe marehemu wetu uzima usio na mwisho
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, Mwanao aliwadhihirishia mitume utayari wake
wa kwenda njia ya mateso. Uyapokee maombi yetu, kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.